News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE CHAWANOA WATAALAMU WA TEHAMA KUCHOCHEA MAGEUZI YA KIDIJITALI

CHUO KIKUU MZUMBE CHAWANOA WATAALAMU WA TEHAMA KUCHOCHEA MAGEUZI YA KIDIJITALI

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kwa kushirikiana na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), kinaendesha mafunzo ya siku tano ya kujengeana uwezo kwa watumishi wa TEHAMA kuanzia tarehe 15 hadi 19 Juni 2026 katika Hoteli ya Morena, Morogoro. Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha watumishi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Chuo, usalama wa taarifa, usimamizi wa vihatarishi na maafa ya TEHAMA, usimamizi wa miradi ya TEHAMA, maboresho ya huduma pamoja na Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano. Akifungua mafunzo hayo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi alisema kuwa TEHAMA ni mhimili muhimu katika kuimarisha utendaji wa taasisi na utoaji wa huduma bora. Aliwataka washiriki kutumia mafunzo hayo kuongeza maarifa, kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kutumia ujuzi watakaoupata kuchangia utekelezaji wa malengo ya kimkakati ya Chuo. Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa HEET upande wa Elimu Jumuishi na Mratibu wa Kituo cha Umahiri katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa Kibunifu, Dkt. Perpetua Kalimasi akizungumza kwa niaba ya Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET, Dkt. Lihoya Chamwali alieleza kuwa mradi huo unaendelea kuunga mkono juhudi za Chuo katika kuimarisha uwezo wa rasilimali watu na maendeleo ya TEHAMA ili kuongeza ubora na ufanisi wa huduma. Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha TEHAMA, Dkt. Mohamed Ghasia alisema watumishi wa TEHAMA wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuibua na kutekeleza bunifu zitakazochochea mageuzi ya kidijitali ndani ya Chuo. Aliwahimiza washiriki kujifunza kwa bidii, kushirikiana na kutumia maarifa watakayoyapata kuboresha huduma, kuimarisha usalama wa mifumo na kuongeza tija katika utendaji kazi. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha ujifunzaji na kuendeleza matumizi sahihi ya teknolojia ndani ya Chuo, ili kuhimili mabadiliko ya kidijitali, kuongeza ufanisi wa huduma na kujiweka katika nafasi bora ya kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu ya juu na Taifa kwa ujumla.

None
None
None
None
None
None
None
None
None