Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu kimefungua rasmi Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 kwa kuwataka watumishi kuendelea kuzingatia uwajibikaji, maadili na utoaji wa huduma bora ili kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa. Maadhimisho hayo yamefanyika tarehe 16 Juni 2026 katika Ukumbi wa Samora, Kampasi Kuu Morogoro, yakiongozwa na kaulimbiu isemayo, “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.” Akifungua maadhimisho hayo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha alisema kaulimbiu ya mwaka huu inapaswa kutafsiriwa kwa vitendo kupitia utendaji kazi unaozingatia uwazi, uadilifu na ushirikishwaji wa wadau katika utoaji wa huduma. Alisisitiza kuwa watumishi wa umma wana nafasi muhimu katika kujenga taasisi imara zinazokidhi matarajio ya wananchi. Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu, Bi. Fatuma Mussa alisema maadhimisho hayo ni jukwaa la kutafakari mchango wa watumishi wa umma, kujifunza na kuimarisha utamaduni wa uwajibikaji. Naye Mkurugenzi wa Afya na Huduma za Kitabibu, Dkt. Rajab Nyangara Mtilly alisisitiza umuhimu wa afya ya akili kwa watumishi, akieleza kuwa ustawi wa akili huongeza ufanisi, umakini na tija mahali pa kazi. Katika ufunguzi huo, Daktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Garvin Kweka aliwasilisha mada kuhusu afya ya akili na uwiano wa maisha, akifafanua kuwa afya ya akili hujengwa katika misingi ya fikira, hisia na tabia. Naye Mchambuzi wa Uwekezaji kutoka Watumishi Housing Investments, CPA Fidelis Lyimo aliwahimiza watumishi kuwa na nidhamu ya kifedha, kujiwekea akiba na kuwekeza kwa ajili ya ustawi wa muda mrefu. Akihitimisha hafla hiyo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro, aliwataka watumishi kutumia elimu waliyoipata kuboresha utendaji kazi na kuendeleza maadili ya utumishi wa umma. Huduma za uchunguzi na ushauri wa afya, elimu ya afya ya akili pamoja na elimu ya fedha na uwekezaji zitaendelea kutolewa kwa watumishi hadi Juni 23, 2026, huku mapokeo ya washiriki yakionyesha utayari mkubwa wa kujifunza na kutumia maarifa hayo kuongeza tija, ustawi binafsi na ubora wa huduma kwa jamii.