Miaka 25 ijayo itafafanuliwa na Dira ya Maendeleo ya Tanzania (TDV) – 2050. TDV 2050 haitabadilisha tu sera za kitaifa, bali pia itatoa mwongozo wa utekelezaji wa mipango ya taasisi, sekta mbalimbali, mikakati na miradi ya maendeleo. Haya yamesemwa tarehe 26 Februari 2025 na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Dkt. Mursali Ally Milanzi katika Hafla ya Washiriki wa Semina ya Kuimarisha Uwezo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini (M&E): Mustakabali wa Tathmini, iliyofanyika nyumbani kwa Balozi wa Ubeligiji nchini Tanzania, Mhe. Balozi Peter Huyghebaert. Semina hii imeandaliwa na Ofisi Maalum ya Tathmini - Ubelgiji, IOB (Chuo Kikuu cha Antwerp) na Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa MU-IOB ICP Connect Dkt. Milanzi alieleza kuwa Dira ya 2050 inajengwa juu ya mafanikio ya Dira ya 2025, huku ikitambua mabadiliko makubwa ya kimataifa kama vile maendeleo ya teknolojia, mabadiliko ya idadi ya watu, changamoto za tabianchi na hali ya kisiasa duniani. Tanzania, ikiwa na rasilimali asilia, nafasi yake ya kijiografia, pamoja na misingi imara ya amani, usalama na utulivu, inatarajia kuwa taifa lenye haki, ustawi, ujumuishi na kujitegemea ifikapo 2050. Katika utawala wa serikali, ufuatiliaji na tathmini ni sehemu ya kawaida ya utendaji, ikiwa chini ya usimamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, ambayo inahusika na kutathmini utendaji wa miradi kwa wananchi na kila wizara ina vitengo maalum vya ufuatiliaji na tathmini kwa ajili ya mipango na miradi ya sekta husika “Ili kuhakikisha utekelezaji wa dira hii, Serikali inapaswa kuimarisha mifumo na miundombinu ya M&E kwa lengo la kufuatilia maendeleo, kutathmini umuhimu wake, na kuhakikisha matokeo yanayopatikana yanatumika kuboresha sera na mipango mingine ya maendeleo. Alieleza Dkt. Milanzi” Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo, Balozi wa Ubeligiji nchini Tanzania, Mhe. Balozi Peter Huyghebaert alisema kuwa Kuimarisha Uwezo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini: Mustakabali wa Tathmini sio tu inalenga kuimarisha uwezo wa kitaifa katika ufuatiliaji na tathmini katika sekta mbalimbali bali inaimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi na nchi. Naye, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sera za Maendeleo (IOB), Prof. Nathalie Holvet amesema kuwa semina hii yenye kaulimbiu “Mustakabali wa Tathmini”, inalenga kuimarisha uwezo wa kitaifa katika ufuatiliaji na tathmini (M&E) na kuendeleza maamuzi yanayozingatia ushahidi katika sekta mbalimbali. Kwa upande wake Mtaalam Maalum wa Tathmini, Ushirikiano wa Maendeleo wa Ubelgiji, Bi. Cécilia De Decker Kupitia semina hii, tunalenga kuchangia katika kuimarisha uwezo wa kitaifa wa ufuatiliaji na tathmini (M&E) pamoja na mitandao yake, huku tukijadili changamoto na fursa za siku zijazo. Tunaamini katika uwezo wa kutumia vyama vya kitaifa vya tathmini ili kuimarisha utaalamu wa kitaifa, ubora wa takwimu, na kutetea kuimarishwa kwa nafasi ya tathmini katika taasisi za kitaifa na mijadala ya sera. Dira ya 2050 inatekelezeka na mustakabali wa Tanzania unatia matumaini endapo tutaweka uwajibikaji, ufanisi na ufanisi katika utungaji sera. M&E itakuwa chombo chenye nguvu katika kujifunza na uwajibikaji, kusaidia kutengeneza sera kwa kutumia ushahidi wa kweli badala ya uvumi au habari potofu. Hivyo, tunahitaji ushirikiano wa pamoja kutoka serikalini, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa M&E inakuwa chombo muhimu cha kuleta maendeleo jumuishi na endelevu.