News-Details

News >Details

MZUMBE YAENDESHA MAFUNZO YA SHERIA ZA KAZI TANZANIA: USIMAMIZI WA MIGOGORO YA KAZI, UKOMO WA AJIRA NA USIMAMIZI WA KESI KIDIGITALI

MZUMBE YAENDESHA MAFUNZO YA SHERIA ZA KAZI TANZANIA: USIMAMIZI WA MIGOGORO YA KAZI, UKOMO WA AJIRA NA USIMAMIZI WA KESI KIDIGITALI

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kitivo cha Sheria kinaendesha mafunzo ya siku tano kuhusu Kuimarisha Uelewa kuhusu Sheria za Kazi Tanzania: Usimamizi wa Migogoro ya Kazi, Ukomo wa Ajira na Usimamizi wa Kesi kwa Mfumo wa Kidijitali yanayofanyika katika Hoteli ya Flomi, mkoani Morogoro kuanzia tarehe 22 – 26 Juni 2026. Mafunzo hayo yanawakutanisha Maafisa Rasilimali Watu, Maafisa Utawala, Mawakili, Washauri wa Sheria wa Ndani wa Taasisi pamoja na Watendaji Wakuu wa Kampuni kutoka taasisi mbalimbali nchini kwa lengo la kuimarisha uelewa na uwezo wa kitaalamu katika usimamizi wa mahusiano ya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na mbinu bora za kisasa za utendaji. Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkuu wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Mzumbe, Mkuu wa Idara ya Masomo ya Sheria wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Mbeya, Dkt. Kennedy Makafu amesema kuwa mazingira ya kazi yanabadilika kwa kasi kutokana na maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya mifumo ya usimamizi, jambo linalohitaji wataalamu kuwa na uelewa wa kina wa sheria za kazi na mbinu za kisasa za kushughulikia changamoto zinazojitokeza mahali pa kazi, Ukomo wa Ajira na Usimamizi wa Kesi kwa Mfumo wa Kidijitali. Kwa upande wake, Mwezeshaji wa Mafunzo na Kaimu Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Wakili Amani Mwalongo amewasilisha mada kuhusu Taratibu za Uendeshaji wa Mashauri ya Kinidhamu Mahali pa Kazi. Wakili Mwalongo ameeleza kuwa waajiri wanapaswa kuzingatia haki na taratibu za kisheria katika mashauri ya kinidhamu ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima na kulinda pande zote. Pia alisisitiza uchunguzi wa kina, kutoa fursa ya kusikilizwa, na kuweka kumbukumbu sahihi ili kuhakikisha maamuzi ya haki, uwazi na uhalali wa kisheria. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha utawala bora katika maeneo ya kazi kwa kuwawezesha washiriki kutumia maarifa na ujuzi walioupata katika kufanya maamuzi sahihi, kuzuia migogoro na kuongeza ufanisi wa taasisi zao katika mazingira ya kazi yanayozidi kuwa ya kidijitali.

None
None
None
None
None
None