Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kitengo cha Umataifishaji na Baraza la Wahitimu kimezindua Mfuko wa Ufadhili wa Masomo wa Jumuiya ya Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe (Mzumbe University Alumni Scholarship Fund) kwa lengo la kuongeza fursa za elimu kwa wanafunzi wenye uhitaji kupitia mchango wa wahitimu na wadau mbalimbali wa maendeleo. Hafla hiyo imefanyika tarehe 24 Juni 2026, Kampasi Kuu Morogoro, ikiambatana na mhadhara wa umma kuhusu Mageuzi ya Kidijitali Yanayozingatia Mahitaji ya Watu na Maboresho ya Utumishi wa Umma nchini Tanzania. Akizungumza katika hafla hiyo, Mgeni Rasmi na mtoa mada wa mhadhara wa umma, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Mhe. Philemon Luhanjo amesema mageuzi ya kidijitali yanapaswa kulenga kuboresha maisha ya wananchi kwa kuimarisha utoaji wa huduma za umma kwa ufanisi, uwazi na uwajibikaji. Alisisitiza umuhimu wa taasisi za elimu ya juu kuandaa wataalamu watakaosimamia mageuzi hayo kwa kuzingatia mahitaji ya jamii. Kwa upande wake, Rais wa Baraza la Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe, CPA Ludovick Utouh amesema mfuko huo unaonesha dhamira ya wahitimu kurejesha mchango wao kwa chuo kwa kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto za kifedha (uhitaji) kufikia malengo yao ya elimu. Awali, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi ameeleza kuwa mfuko huo utaimarisha mshikamano kati ya chuo na wahitimu wake. Naye Mkurugenzi wa Kitengo cha Umataifishaji na Baraza la Wahitimu, Dkt. Lucy Massoi amesisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kuendeleza elimu na umoja wa wahitimu na wanafunzi wanaoendelea na masomo, huku Kaimu Amidi wa Skuli ya Utawala wa Umma na Menejimenti, Prof. Mackfallen Anasel akieleza mchango wa Skuli hiyo katika kuandaa wataalamu watakao saidia mageuzi ya kidijitali na utumishi wa umma. Aidha, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro ameeleza kuwa mfuko huo utaimarisha fursa za elimu kwa wanafunzi wenye uhitaji na kuendeleza utamaduni wa wahitimu kurejesha mchango wao kwa chuo. Uzinduzi wa mfuko huo unatarajiwa kuongeza fursa za elimu kwa wanafunzi wenye uhitaji na kuimarisha mchango wa wahitimu katika maendeleo ya Chuo Kikuu Mzumbe na taifa kwa ujumla.