News-Details

News >Details

DIRISHA LA UDAHILI LIPO WAZI: MZUMBE KUENDELEA KUZALISHA WAHITIMU WENYE USHINDANI KATIKA SOKO LA AJIRA

DIRISHA LA UDAHILI LIPO WAZI: MZUMBE KUENDELEA KUZALISHA WAHITIMU WENYE USHINDANI KATIKA SOKO LA AJIRA

Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kuwekeza katika utoaji wa elimu bora na inayozingatia mahitaji ya soko la ajira ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi, sambamba na kuwawezesha kujiajiri kupitia taaluma mbalimbali zinazotolewa na chuo hicho. Akizungumza katika Banda la Chuo wakati wa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam - Sabasaba 2026, Mkuu wa Idara ya Udahili wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Michael Mangula amesema dirisha la udahili kwa ngazi za Astashahada, Stashahada, Shahada za Uzamili na Uzamivu limefunguliwa na litaendelea hadi Oktoba 2026, huku udahili wa Shahada za Awali umefunguliwa rasmi Julai 10, 2026 kwa kuzingatia kalenda ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania. Dkt. Mangula amesema Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kutoa programu zenye ubora wa kitaaluma katika maeneo mbalimbali ikiwemo Uhasibu na Fedha, Uongozi na Utawala, Sheria, Biashara na Ujasiriamali, Uchumi, Sayansi na Teknolojia, Usimamizi wa Mazingira, Ualimu, Menejimenti ya Mifumo ya Afya, Ufuatiliaji na Tathmini pamoja na Usimamizi wa Miradi ambazo zimeendelea kuzalisha wahitimu wanaokidhi mahitaji ya waajiri, kuwawezesha wanahitimu kujiajili na hivyo kuchangia katika maendeleo ya Taifa. Ameongeza kuwa Banda la Chuo linaendelea kutoa huduma za udahili bila malipo, ambapo wataalamu wanawasaidia waombaji kupata ushauri wa kitaaluma na kuchagua programu zinazolingana na sifa na malengo yao ya taaluma. Aidha, amesema Chuo kinaendelea kupanua huduma za elimu ya juu kupitia ujenzi wa Kampasi mpya ya Tanga unaotekelezwa chini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), hatua inayolenga kuongeza nafasi za udahili na kupeleka elimu bora karibu zaidi na wananchi. Dkt. Mangula amewahimiza wanafunzi, wazazi na wadau mbalimbali kutembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere ili kupata taarifa za udahili, ushauri wa kitaaluma na huduma nyingine zinazotolewa na Chuo. Aidha, amebainisha kuwa huduma za udahili zinaendelea kutolewa kwa njia ya mtandao kupitia ‘Mzumbe Admission Portal’, ambapo waombaji wanaweza kuwasilisha maombi yao na kupata usaidizi kutoka kwa wataalamu wa masuala ya udahili wa Chuo. Jiunge na Chuo Kikuu Mzumbe sasa, mahali ambako maarifa hujenga kujiamini, ujuzi huibua fursa na kuelekea kutimiza ndoto zako. Karibu Chuo Kikuu Mzumbe, "Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu

None
None
None
None
None
None
None