News-Details

News >Details

MZUMBE YATUMIA SABASABA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA WAHITIMU, KUHAMASISHA MFUKO WA UFADHILI WA MASOMO

MZUMBE YATUMIA SABASABA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA WAHITIMU, KUHAMASISHA MFUKO WA UFADHILI WA MASOMO

Ushiriki wa Chuo Kikuu Mzumbe katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam - Sabasaba 2026 yanaendelea kuanzia Juni 28 – Julai 13 umeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano na wahitimu (Alumni) na wadau mbalimbali, sambamba na kuhamasisha ushiriki wao katika Mfuko wa Ufadhili wa Masomo wa Jumuiya ya Wahitimu wa Chuo Kikuu Mzumbe (Mzumbe University Alumni Scholarship Fund). Mfuko huo ulianzishwa na Chuo kupitia Kitengo cha Umataifishaji na Baraza la Wahitimu, ukiwa na lengo la kuongeza fursa za elimu kwa wanafunzi wenye uhitaji kupitia michango ya wahitimu na wadau wa maendeleo. Ulizinduliwa tarehe 24 Juni 2026, Kampasi Kuu Morogoro, katika hafla iliyoambatana na mhadhara wa umma kuhusu Mageuzi ya Kidijitali Yanayozingatia Mahitaji ya Watu na Maboresho ya Utumishi wa Umma nchini Tanzania, uliotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Mhe. Philemon Luhanjo. Katika maonesho haya, Mratibu wa Baraza la Wahitimu na Umataifishaji wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bi. Candid Katalaihya amekuwa akitoa maelezo kwa wahitimu wanaotembelea banda la chuo kuhusu umuhimu wa mfuko huo, akieleza kuwa umeanzishwa ili kuhakikisha wanafunzi wenye changamoto za kifedha wanapata fursa ya kuendelea na masomo na kutimiza ndoto zao. Amesisitiza kuwa mchango wa wahitimu ni njia ya kurejesha fadhila kwa Chuo na kuwekeza katika maendeleo ya vizazi vijavyo. Bi. Katalaiya pia amewahamasisha wahitimu na wadau wengine kujiunga na juhudi hizo kwa kuchangia kupitia Namba ya Akaunti ya CRDB: 01500001NAR00, Jina: Mzumbe University Alumni Scholarship Fund, akieleza kuwa kila mchango, mkubwa au mdogo, una nafasi ya kubadili maisha ya mwanafunzi. Baadhi ya wahitimu waliotembelea banda hilo wameupokea mpango huo kwa matumaini makubwa, wakieleza kuwa ni hatua ya kihistoria inayowapa fursa ya kushiriki moja kwa moja katika kuwainua wanafunzi wenye uhitaji. Wamesema mfuko huo unaimarisha mshikamano wa wahitimu na kuendeleza utamaduni wa kusaidiana, huku wakitoa wito kwa wahitimu wote wa Chuo Kikuu Mzumbe, taasisi na wadau wengine kujiunga na mpango huo kwa kutoa michango itakayowezesha wanafunzi wengi zaidi kutimiza ndoto zao za elimu. Maonesho ya Sabasaba kwa Chuo Kikuu Mzumbe ni jukwaa muhimu katika kuimarisha mtandao wa wahitimu na wadau, kutangaza fursa zake za kitaaluma na kuhamasisha ushiriki wa pamoja katika kuwezesha vijana kupata elimu bora. Ushirikiano huu unaweka msingi imara wa kujenga kizazi chenye maarifa, ujuzi na uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na maendeleo ya Taifa.

None
None
None
None
None
None
None
None
None