News-Details

News >Details

MZUMBE YAIMARISHA JUHUDI ZA KUKUZA KISWAHILI NJE YA MIPAKA YA TANZANIA

MZUMBE YAIMARISHA JUHUDI ZA KUKUZA KISWAHILI NJE YA MIPAKA YA TANZANIA

Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kudhihirisha mchango wake katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili kimataifa, huku Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro, akisisitiza kuwa Kiswahili si lugha ya mawasiliano pekee, bali ni nyenzo muhimu ya kujenga amani, kuimarisha mshikamano wa mataifa na kuchochea diplomasia ya kiuchumi pamoja na maendeleo endelevu barani Afrika. Prof. Hawa alitoa kauli hiyo alipokuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yaliyoandaliwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi na kufanyika katika Chuo Kikuu cha Emmanuel, Lilongwe, tarehe 24 Julai 2026. Maadhimisho hayo, yaliyoongozwa na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola, yalifanyika chini ya kaulimbiu "Kiswahili kwa Amani, Mshikamano na Diplomasia ya Kiuchumi Duniani", na kuwakutanisha wanafunzi, wahadhiri, watafiti, wadau wa elimu pamoja na wageni mbalimbali kwa ajili ya kusherehekea mchango wa Kiswahili katika kuimarisha utambulisho wa Afrika, umoja wa mataifa na ushirikiano wa kimataifa. Akihutubia washiriki, Prof. Hawa alisema kuongezeka kwa matumizi ya Kiswahili katika mataifa mbalimbali ni kielelezo cha kuimarika kwa hadhi ya lugha hiyo duniani. Alibainisha kuwa Kiswahili kimeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kukuza elimu, kurahisisha biashara, kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kuendeleza diplomasia, hivyo kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi ya Bara la Afrika. Akizungumzia mchango wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kukuza Kiswahili kimataifa, Prof. Hawa alisema chuo kinaendelea kupanua ushirikiano wake wa kitaaluma na taasisi mbalimbali za elimu nje ya Tanzania. Alieleza kuwa kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo Kikuu cha Malawi (UNIMA), mhadhiri kutoka Mzumbe, Dkt. Maria Kanigi, anafundisha lugha ya Kiswahili kama mhadhiri mgeni, huku programu hiyo ikiwa tayari imevutia wanafunzi 17, hatua inayoashiria kuongezeka kwa hamasa ya kujifunza Kiswahili nchini Malawi. Prof. Hawa aliongeza kuwa mafanikio hayo yanaonesha namna Chuo Kikuu Mzumbe kinavyoendelea kuchangia juhudi za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania za kukuza hadhi ya Kiswahili kama lugha ya elimu, diplomasia na maendeleo katika jukwaa la kimataifa kupitia ushirikiano wa kitaaluma na ubadilishanaji wa wataalamu. Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Mhe. Agnes Kayola, alikipongeza Chuo Kikuu cha Emmanuel kwa kuendelea kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania katika juhudi za kukuza lugha ya Kiswahili. Alisema chuo hicho kimekuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kwa miaka mitatu mfululizo, jambo linalodhihirisha dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano wa kielimu, kitamaduni na kidiplomasia kati ya Tanzania na Malawi. Ingawa Siku ya Kiswahili Duniani huadhimishwa rasmi kila mwaka tarehe 7 Julai, Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi uliadhimisha siku hiyo tarehe 24 Julai 2026, ukiendelea kuhamasisha matumizi ya Kiswahili kama lugha ya mawasiliano ya kimataifa, urithi wa kitamaduni na nyenzo ya kuimarisha ushirikiano wa maendeleo. Maadhimisho hayo yameendelea kudhihirisha kuwa Kiswahili kinaendelea kupata nafasi kubwa katika jukwaa la kimataifa, huku taasisi za elimu ya juu zikibaki kuwa nguzo muhimu katika safari hiyo. Kupitia ushiriki wake katika hafla hiyo, Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kuchangia katika kuimarisha elimu, kukuza lugha ya Kiswahili na kujenga ushirikiano wa kimataifa wenye tija kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla.

None
None
None
None
None
None
None