News-Details

News >Details

MZUMBE YAIMARISHA HUDUMA ZA UPASUAJI NA KINGA DHIDI YA VVU

MZUMBE YAIMARISHA HUDUMA ZA UPASUAJI NA KINGA DHIDI YA VVU

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudhibiti VVU/UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza Chuo Kikuu Mzumbe, ameongoza wajumbe wa Kamati hiyo kufanya ukaguzi wa miundombinu na huduma za afya zinazotolewa na Chuo, ikiwemo jengo jipya la Upasuaji pamoja na Mashine ya Kidijitali ya Kondomu na Vipimo vya JIPIME (VVU), katika Kituo cha Afya Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro, leo tarehe 12 Agosti 2026. Katika ziara hiyo, Prof. Mwegoha amekagua kwa kina jengo jipya la Upasuaji, akipitia maeneo mbalimbali ya jengo hilo pamoja na vifaa vilivyowekwa kwa ajili ya kuwezesha utoaji wa huduma za upasuaji. Miongoni mwa maeneo yaliyokaguliwa ni chumba cha upasuaji (Theatre Room) pamoja na vifaa maalumu vinavyotumika katika huduma hiyo, ikiwemo mashine ya nusu kaputi (Anaesthesia Machine). Ukaguzi huo umewezesha kamati kujionea hatua iliyofikiwa katika maandalizi ya jengo hilo na namna miundombinu pamoja na vifaa vilivyopo vitakavyosaidia kuongeza uwezo wa Kituo cha Afya katika kutoa huduma za kitabibu kwa wanafunzi, watumishi na jamii inayozunguka Chuo. Mbali na jengo hilo la Upasuaji, Prof. Mwegoha amekagua pia Mashine ya Kidijitali ya Kondomu na Vipimo vya JIPIME, iliyowekwa katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa msaada wa TACAIDS, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma na vifaa vya kinga dhidi ya VVU pamoja na huduma za kujipima. Mashine hiyo inatoa fursa kwa wanajumuiya ya Chuo kupata kondomu na huduma za vipimo vya kujipima kwa njia rahisi na yenye faragha, hatua inayolenga kuhamasisha zaidi matumizi ya huduma za kinga na upimaji wa VVU miongoni mwa wanafunzi na jamii ya Chuo kwa ujumla. Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Mwegoha amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha huduma za afya ndani ya Chuo, akieleza kuwa mazingira bora ya afya ni sehemu muhimu katika kuhakikisha wanafunzi na watumishi wanatekeleza majukumu yao ya kielimu na kikazi katika mazingira salama na yenye ustawi. Ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati ya Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kufuatilia, kutathmini na kuimarisha hatua mbalimbali zinazolenga kulinda afya na ustawi wa wanajumuiya ya Chuo. Uwekezaji katika jengo jipya la Upasuaji pamoja na matumizi ya teknolojia katika huduma za afya unaendelea kuonesha jitihada za Chuo Kikuu Mzumbe katika kuboresha huduma zake za afya na kuhakikisha wanajumuiya wake wanapata huduma muhimu kwa wakati, kwa usalama na katika mazingira yanayozingatia mahitaji yao.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None