Chuo Kikuu Mzumbe kimepiga hatua kubwa katika safari ya kuimarisha na kupanua huduma za elimu ya juu baada ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kuthibitisha kuwa Kampasi ya Tanga imepata ithibati, hatua inayoweka msingi muhimu kwa Kampasi hiyo kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake kwa kuzingatia viwango vya kitaifa vya elimu ya juu. Hatua hiyo imethibitishwa leo, tarehe 21 Agosti 2026, katika Kampasi ya Tanga iliyopo Gombero, Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, na Mwenyekiti wa TCU, Prof. Makenya Maboko, wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya Kampasi hiyo akiwa ameambatana na Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa. Katika ziara hiyo, viongozi hao wa TCU wamekagua kwa kina miundombinu na mazingira mbalimbali ya Kampasi ya Tanga, huku wakipata fursa ya kujionea kwa vitendo uwekezaji unaoendelea kufanywa na Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET). Ukaguzi huo umejikita katika kutathmini maendeleo ya miundombinu, maandalizi ya mazingira ya kujifunzia na kufundishia pamoja na hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Chuo kuhakikisha Kampasi hiyo inakuwa na uwezo wa kutoa huduma za elimu ya juu kwa kuzingatia viwango vya ubora vinavyotakiwa. Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Prof. Makenya Maboko amesema Kampasi ya Tanga tayari imepata ithibati kutoka TCU, jambo linaloashiria kuwa hatua muhimu zimekamilika katika kuhakikisha Kampasi hiyo inakidhi matakwa na viwango vilivyowekwa kwa taasisi za elimu ya juu nchini. Hatua hiyo ni muhimu kwa Chuo Kikuu Mzumbe katika kuendeleza azma yake ya kupanua wigo wa utoaji wa elimu ya juu na kuhakikisha uwekezaji unaofanyika Kampasi ya Tanga unazaa matokeo yenye tija kwa Chuo, jamii na Taifa kwa ujumla. Ziara hiyo imefanyika katika kipindi ambacho Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea kutekeleza kwa kasi mpango wake wa kuimarisha miundombinu na kuongeza uwezo wa utoaji wa elimu kupitia Mradi wa HEET, unaolenga kuwezesha taasisi za elimu ya juu nchini kuwa na mazingira bora ya kujifunzia, kufundishia, kufanya utafiti na kutoa huduma za kitaalamu. Akiongoza ujumbe wa Chuo wakati wa ziara hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, ameambatana na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Hawa Tundui Petro, pamoja na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, baadhi ya viongozi waandamizi wa Chuo na waratibu wa Mradi wa HEET. Kwa wananchi wa Tanga na mikoa ya jirani, hatua hiyo inabeba matarajio mapya ya kuongezeka kwa fursa za elimu ya juu na huduma za kitaalamu karibu na maeneo yao. Kampasi ya Tanga inapoendelea kukua, Chuo Kikuu Mzumbe kinalenga kutumia uwepo wake katika ukanda huo kuimarisha uzalishaji wa maarifa, utafiti na ubunifu unaolenga kutatua changamoto halisi za jamii, sambamba na kuandaa wataalamu wenye uwezo wa kushiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa kisasa na unaozingatia maarifa.