Katika hatua ya kuimarisha weledi na uwezo wa wataalamu katika uendeshaji wa shughuli rasmi, Chuo Kikuu Mzumbe kimeendesha mafunzo ya muda mfupi ya siku tano kuhusu Itifaki na Uratibu wa Matukio, yanayolenga kuwapa washiriki maarifa na ujuzi muhimu wa kuhakikisha matukio yanaandaliwa na kusimamiwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia taratibu za kitaalamu. Mafunzo hayo yameanza leo Agosti 31, 2026, Hoteli ya Edema mkoani Morogoro, na yataendelea hadi Septemba 4, 2026, yakijikita katika kujenga uelewa wa kina kuhusu misingi ya itifaki, maadili, mwenendo wa kitaalamu na mbinu bora za kusimamia matukio katika mazingira rasmi na ya taasisi. Akiongoza mafunzo ya siku ya kwanza, Mwezeshaji ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Stephen Nalaila aliwapatia washiriki maarifa kuhusu misingi ya itifaki, maadili na mwenendo wa kitaalamu, akieleza umuhimu wa kuelewa dhana, kanuni na misingi inayosimamia utekelezaji wa shughuli na matukio mbalimbali. Katika mafunzo hayo, washiriki walijifunza kuhusu kanuni za itifaki na maadili katika matukio rasmi na ya taasisi, pamoja na mambo muhimu yanayojenga taswira ya kitaalamu, yakiwemo namna ya kuvaa, mwenendo binafsi, mawasiliano, salamu na utambulishaji sahihi wa watu katika mazingira rasmi. Aidha, kupitia sehemu ya mafunzo ya vitendo, washiriki walipata fursa ya kuchambua na kujadili mazingira mbalimbali yanayohusiana na utekelezaji wa itifaki, hususan upangaji wa viti, utaratibu wa wageni na namna ya kupokea na kuwahudumia wageni kwa kuzingatia hadhi na taratibu zinazotakiwa. Mafunzo hayo ya siku tano ni sehemu ya mchango wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kuendelea kutoa mafunzo yanayojibu mahitaji ya wataalamu na taasisi mbalimbali, kwa kuwajengea washiriki uwezo unaoweza kutumika moja kwa moja katika mazingira yao ya kazi na kuchangia utoaji wa huduma bora.