News-Details

News >Details

KIHENZILE AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA SEKTA YA UCHUKUZI NA MNYORORO WA UGAVI BARANI AFRIKA

KIHENZILE AHIMIZA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KUIMARISHA SEKTA YA UCHUKUZI NA MNYORORO WA UGAVI BARANI AFRIKA

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Kihenzile, ameeleza kuwa mifumo bora ya usafirishaji ndiyo uti wa mgongo unaounganisha wazalishaji, masoko na fursa za kiuchumi barani Afrika. Kihenzile amebainisha hayo wakati akifungua rasmi Mkutano wa 8 wa Afrika wa Uendeshaji na Usimamizi wa Mnyororo wa Ugavi (ACOSCM) leo Septemba 22, 2026, katika Hoteli ya Mount Meru, Arusha. Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, Kihenzile amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika miundombinu ya kimkakati ikiwemo reli, bandari, pamoja na usafiri wa anga na majini ili kuwezesha biashara na kukuza sekta ya utalii. Hata hivyo, alisisitiza kuwa miundombinu pekee haitoshi bila kuwepo kwa mabadiliko ya kidijitali na matumizi ya teknolojia mpya kama Akili Mnemba katika ufuatiliaji wa mizigo na ubadilishanaji wa taarifa. Kwa upande wake, Mgeni Maalumu katika Mkutano huo Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amebainisha kuwa lengo la mkutano huo ni kujenga ushirikiano thabiti na wa kimkakati unaounganisha vyuo vikuu na sekta ya viwanda katika nyanja za elimu, utafiti, na ubunifu. Prof. Mwegoha amesema kuwa changamoto za kidunia kama mabadiliko ya tabianchi, msukosuko wa kiuchumi, na majanga ya afya zinaendelea kuathiri mifumo ya ugavi barani Afrika. Alifafanua kuwa kujenga minyororo ya ugavi yenye ustahimilivu kunahitaji zaidi ya miundombinu na teknolojia kunahitaji bali rasilimali watu wenye ujuzi wa hali ya juu, tafiti za kuaminika, na taasisi zinazosimamia kwa madhubuti. Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Mkutano huo ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe - Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Hawa Tundui Petro, alisema mkutano wa mwaka huu imejikita katika mada za kimkakati kama matumizi ya Akili Mnemba (AI), mifumo endelevu ya ugavi katika huduma za afya, mfumo wa chakula na kilimo, pamoja na usafiri rafiki kwa mazingira. Prof. Hawa alitoa wito kwa vyuo vikuu kutathmini mara kwa mara mitaala na mbinu za ufundishaji ili kuandaa wahitimu wenye umahiri wa kidijitali, fikra changanuzi, na uongozi wenye maadili unaoendana na mabadiliko ya haraka ya soko la ajira. Matokeo na mapendekezo yatakayopatikana katika siku hizi mbili yanatarajiwa kutoa dira mpya katika mnyororo wa ugavi kama njia pekee ya kuijenga Afrika yenye ustahimilivu wa kiuchumi na kugeuza tafiti za kitaaluma kuwa suluhisho kwa sekta husika.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None