News-Details

News >Details

MAHAFALI YA 25 YA MZUMBE YAADHIMISHA MAFANIKIO YA CHUO NA WAHITIMU

MAHAFALI YA 25 YA MZUMBE YAADHIMISHA MAFANIKIO YA CHUO NA WAHITIMU

Chuo Kikuu Mzumbe kimefanya Mahafali ya 25 leo, tarehe 22 Oktoba 2026, katika Kampasi Kuu ya Morogoro, yakiongozwa na Mgeni Rasmi ambaye pia ni Mkuu wa Chuo hicho, Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein. Mahafali hayo yamekuwa fursa ya kutambua mafanikio ya Chuo katika kuimarisha ubora wa elimu, kukuza ubunifu na kupanua fursa za elimu ya juu, huku viongozi wakisisitiza wajibu wa wahitimu kutumia maarifa yao kwa manufaa ya jamii na taifa. Akizungumza katika hotuba yake, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, amewapongeza wahitimu kwa juhudi, nidhamu na uvumilivu waliouonesha katika safari yao ya kitaaluma. Amewahimiza kuendeleza ubunifu, kuzingatia maadili na kutumia maarifa pamoja na teknolojia, ikiwemo Akili Mnemba (AI), kwa uwajibikaji ili kuchangia maendeleo ya jamii na taifa. Aidha, amesisitiza umuhimu wa mshikamano na uwajibikaji katika kuendeleza ubora wa Chuo Kikuu Mzumbe. Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, akizungumza katika hotuba yake, amesema Chuo kimeendelea kutekeleza mipango yake ya kimkakati, ambapo katika mwaka wa fedha 2025/2026 kilifikia wastani wa asilimia 89.58 ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Tano. Ameeleza kuwa chuo kinaendelea kuboresha programu za masomo ili ziendane na mahitaji ya soko la ajira na vipaumbele vya maendeleo ya taifa, huku kikitumia utaalamu wa watumishi wake kutoa mafunzo na huduma za ushauri wa kitaalamu zinazosaidia kutatua changamoto za jamii. Prof. Mwegoha pia amebainisha juhudi za Chuo katika kukuza ubunifu na ujasiriamali, ambapo zaidi ya wanafunzi 200 walipata mafunzo ya kubuni na kuendeleza mawazo bunifu mwaka 2026. Ameeleza kuwa Chuo kinaimarisha matumizi ya TEHAMA katika shughuli za kitaaluma na kiutawala, sambamba na kupanua fursa za elimu ya juu kupitia Kampasi ya Mkinga, Tanga, ambayo miundombinu yake ya awamu ya kwanza imekamilika kwa zaidi ya asilimia 98 na imepata ithibati ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU). Chuo kinatarajia kuanza shughuli za kitaaluma katika kampasi hiyo mwaka wa masomo 2027/2028. Kwa upande wa wahitimu, Mhitimu Bora wa Chuo Kikuu Mzumbe kwa mwaka 2026, Bw. Collins Mulemwa, akitoa hotuba ya shukrani kwa niaba ya wahitimu wenzake, amewashukuru uongozi wa Chuo, wahadhiri, watumishi, wazazi na walezi kwa mchango wao katika kufanikisha safari yao ya kitaaluma. Amewahimiza wanafunzi wanaoendelea na masomo kuzingatia nidhamu, uvumilivu na bidii, akisisitiza kuwa kuhitimu ni mwanzo wa safari mpya ya kujifunza na kutumia maarifa kwa weledi na uadilifu katika kuitumikia jamii. Mahafali hayo yameonesha dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe ya kuendeleza elimu yenye ubora na kuandaa wahitimu wenye uwezo wa kutumia maarifa kutatua changamoto za jamii. Ujumbe wa viongozi na wahitimu umeweka msisitizo katika ubunifu, maadili na uwajibikaji kama misingi ya kuchangia maendeleo ya watu na taifa, kwa kuzingatia kaulimbiu ya Chuo, “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.”

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None