News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE CHASHIRIKI KIKAO CHA TATHMINI YA MRADI WA HEET KITAIFA

CHUO KIKUU MZUMBE CHASHIRIKI KIKAO CHA TATHMINI YA MRADI WA HEET KITAIFA

Chuo Kikuu Mzumbe kimeshiriki katika kikao cha tathmini ya Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) kati ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Waratibu wa Mradi wa HEET kutoka Taasisi 22 za Elimu ya Juu nchini Tanzania. Kikao hiki kinalenga kupokea na kujadili maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo katika kila taasisi husika. Kikao hiki cha siku tatu, kinachofanyika kuanzia tarehe 10 hadi 12 Machi 2025 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kinahusisha majadiliano ya kina kuhusu maendeleo ya mradi, changamoto zinazokabili utekelezaji wake, na mikakati ya kuboresha utekelezaji wake kwa mujibu wa vigezo vya Benki ya Dunia, ambayo ni mfadhili mkuu wa mradi huo. Akifungua kikao hicho, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa HEET kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Kenneth Hosea, amewahimiza waratibu wa mradi katika taasisi husika kuhakikisha kuwa mapendekezo na maboresho yaliyotolewa yanatekelezwa ipasavyo. Amesisitiza kuwa tathmini na ufuatiliaji wa mradi ni muhimu ili kuhakikisha kuwa mradi unatekelezwa kwa wakati na kwa ufanisi, huku changamoto zilizojitokeza zikitatuliwa kwa njia endelevu. Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa HEET anayehusika na Ufuatiliaji na Tathmini katika Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Lihoya Chamwali, akiwasilisha ripoti ya utekelezaji wa mradi kwa niaba ya Mratibu Mkuu wa HEET katika chuo hicho, ameeleza kuwa ripoti hiyo imejikita katika maeneo mbalimbali muhimu. Miongoni mwa maeneo hayo ni maendeleo ya utekelezaji wa tahadhari za mazingira na jamii na hatua zilizochukuliwa kurekebisha changamoto; maendeleo ya ujenzi, ukarabati na uwekaji wa vifaa katika vituo vya elimu ya juu; viashiria vya mfumo wa matokeo; filamu inayoonyesha madhara chanya ya mradi; mikakati ya kuajiri wafanyakazi wapya kwa kampasi mpya zilizoanzishwa; uundaji wa mitaala mipya; na uhusiano kati ya vyuo vikuu na sekta ya viwanda. Kikao hiki kinatarajiwa kuleta mwendelezo mzuri katika utekelezaji wa mradi wa HEET kwa kuhakikisha taasisi husika zinazingatia viwango vilivyoainishwa ili kufanikisha lengo kuu la kuboresha elimu ya juu kwa maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania.

None
None
None
None
None
None
None
None
None