Katika kuendeleza dhima ya kuimarisha Ushirikiano na Mahusiano ya Kitasnia, Chuo Kikuu Mzumbe kimesaini Hati ya Makubaliano ya Ushirikiano na Chama cha Wafugaji Tanzania. Hafla ya utiaji saini imefanyika tarehe 18 Machi 2025, Kampasi Kuu Morogoro ikijumuisha viongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe na viongozi wa Chama cha Wafugaji Tanzania. Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha amekipongeza Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Mahusiano ya Kitasnia kwa kazi nzuri huku akitanabaisha kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kinatoa elimu katika nyanja mbalimbali ikiwemo Uongozi na Menejimenti, Uchumi na fedha, Biashara, TEHAMA, Sheria, Ualimu, Mipango, Ugavi, Mazingira, Masoko, Hisabati na Takwimu tumizi, Usimamizi wa Uandisi wa Viwanda na Uzalishaji, Uvumbuzi na Ujasiriamali. “Sisi tupo tayari kutumia taaluma zetu hizi na tafiti ili kuchagiza maendeleo ya Chuo, Chama cha Wafugaji pamoja na Taifa kwa ujumla”. Alisema Prof. Mwegoha. Kwa upande wake Katibu wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Bw. Mathayo Daniel ameeleza kuwa wamevutiwa na huduma za kitaalamu katika maeneo mbalimbali ya kitaaluma huku akibainisha kuwa watajikita hasa kushirikiana katika masuala ya uongozi, TEHAMA, Sheria, Biashara, Masoko na Ujasiriamali ili kuweza kuwasaidia wafugaji kuondokana na ufugaji wa mazoea na kuboresha mbinu za ufugaji wa kisasa wenye tija kwa wafugaji na Taifa. Awali akizungumza wakati wa ufunguzi wa hafla hiyo, Meneja wa Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Mahusiano ya Kitasnia, Prof. Emmanuel Chao ameeleza kuwa makubaliano hayo yanalenga kuongeza thamani ya bidhaa za wafugaji Tanzania, Kuhimarisha shughuli za utafiti katika masoko na namna bora ya kuandaa bidhaa za wafugaji, Kuibua miradi ya pamoja, mafunzo pamoja na huduma za ushauri wa kitaalamu kuhusu shughuli za ufugaji. Naye Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Eliza Mwakasangula alisisitiza kuhusu umuhimu wa kuwa na hati ya makubaliano ya ushirikiano inayotekelezeka ili kuleta tija kwa pande zote mbili na Taifa.