Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Skuli ya Biashara kimeendesha mafunzo maalum ya uwezeshaji wa kifedha kwa mafundi wa fani mbalimbali katika Kata ya Mzumbe. Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za chuo kurudisha kwa jamii (Corporate social responsibility)kwa kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na maarifa yanayotolewa chuoni hapo. Akifungua mafunzo hayo rasmi, Amidi wa Skuli ya Biashara, Dkt. Gabriel Komba, aliwapongeza mafundi waliojitokeza kushiriki na kuwatia moyo kuwa maarifa watakayoyapata yataongeza ufanisi katika kazi zao na kuchangia maendeleo yao kwa ujumla. "Chuo Kikuu Mzumbe kimeanzisha programu hii kama sehemu ya wajibu wetu kwa jamii. Tunataka mafundi na wakazi wa maeneo ya jirani wanufaike moja kwa moja na elimu inayotolewa hapa, hususan katika masuala ya fedha na biashara," alisema Dkt. Komba. Naye, Dkt. Juma Buhimila, mmoja wa wawezeshaji, aliwafundisha washiriki juu ya usimamizi wa mapato na matumizi, akibainisha kuwa matumizi yasiyo na mpangilio mzuri yanaweza kusababisha kufilisika. Pia, alisisitiza umuhimu wa kuweka kumbukumbu sahihi za mapato na matumizi ili kuhakikisha mafundi hawatumii mtaji wao wakidhani ni faida. “Kuna matumizi mengi ambayo unayaingia lakini kwa sababu ya kutoyatambua, unashindwa kuyaweka kwenye hesabu zako. Usipofanya hivyo, unaweza kudhani unapata faida kubwa na kuitumia, kumbe unakula mtaji na hatimaye kufunga biashara yako,” alieleza Dkt. Buhimila. Vilevile, Dkt. Moshi James Derefa alizungumzia umuhimu wa kuwa na ujuzi wa fedha, ikiwa ni pamoja na mbinu za kuweka akiba, kuwekeza kwa faida, na kushirikiana katika masuala ya kifedha. Pia, aliwafundisha tabia muhimu zinazoweza kusaidia kufanikisha malengo yao ya kifedha, kama vile nidhamu ya matumizi, uwekaji wa akiba kupitia benki, vikundi vya kifedha (VICOBA), na mitandao ya simu, pamoja na mbinu za upanuzi wa mitaji na njia za kupata ufadhili wa biashara. Kadhalika, Mtendaji wa Kijiji cha Changarawe, Bi. Teddy Eustach, aliwahimiza mafundi hao kujiunga na mfumo wa serikali wa ununuzi na ugavi (NEST), akibainisha kuwa serikali hutangaza zabuni nyingi kupitia mfumo huo, na wale waliojisajili wana nafasi kubwa ya kunufaika nazo. Kwa upande wake, Meneja wa Benki ya CRDB tawi la Mzumbe, Bi. Lucia Lumala, alilishukuru Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuandaa mafunzo haya na kupongeza mafundi kwa mwitikio wao mkubwa. Pia, alieleza kuwa ni muhimu kwa mafundi na wajasiriamali kuwa na mpangilio mzuri wa kifedha ili kuhakikisha fedha wanazopata zinatumika kwa tija. “Ni muhimu kama fundi au mjasiriamali mdogo kuwa na mgawanyo mzuri wa mapato na matumizi. Kila fedha unayoipata lazima iwe na matumizi yaliyopangwa vizuri ili kuepuka matatizo ya kifedha,” alisema Bi. Lumala. Mafunzo haya, ambayo yalihusisha zaidi mafunzo ya vitendo, yamepokelewa vyema na mafundi hao, kiasi cha wao kuamua kuanzisha umoja wa kusaidiana na hatimaye kuunda VICOBA yao kwa ajili ya maendeleo ya biashara zao. Akihitimisha mafunzo hayo, Dkt. Moshi James aliwashukuru washiriki kwa ushirikiano wao na kuwasihi kuyatendea kazi maarifa waliyopata ili kuboresha maisha yao na ustawi wa jamii kwa ujumla.