Chuo Kikuu Mzumbe chenye Mkataba wa Makubaliano na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) wa kutoa mafunzo ya mifumo tumizi ya TEHAMA nchini kwa Taasisi za Umma, kimeendesha mafunzo kwa vitendo ya mfumo wa Ofisi Mtandao na Mfumo wa Barua pepe za Serikali kwa watumishi wa Umma kwa kada za Afisa Utumishi/Utawala, Afisa TEHAMA na Watumishi wa Masijala. Mafunzo haya yaliyojumuisha washiriki takribani 30 kutoka taasisi mbalimbali yamefanyika kwa siku tano kuanzia Machi 17 – 21, 2025, Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine Kampasi ya Solomon Mahlangu (Mazimbu) yakiratibiwa na kusimamiwa na Chuo Kikuu Mzumbe. Akizungumza wakati wa kuhitimishwa kwa mafunzo hayo Amidi wa Skuli ya Utawala wa Umma na Menejimenti Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Idda Lyatonga Swai (Kwa niaba ya Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo - Taaluma, Utafiti na Ushauri, Prof. Eliza Mwakasangula), amewapongeza washiriki wa mafunzo hayo kwa kuona umuhimu wa kujifunza zaidi na kuwataka kwenda kutumia elimu hiyo kuongeza ufanisi katika maeneo yao ya kazi. “Chuo Kikuu Mzumbe tunatoa huduma za mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa kada mbalimbali hivyo, nitoe wito kwenu kutumia fursa hii kuendelea kuja na kujifunza kutoka Chuo Kikuu Mzumbe” Alisisitiza Dkt. Swai. Kwa upande wake mkufunzi wa mafunzo hayo na mkufunzi wa mifumo tumizi ya Serikali ambaye pia ni Afisa TEHAMA Mwandamizi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Alexander Benedicto ameeleza lengo la mafunzo haya ni kutoa uelewa wa mfumo kwa kina za moduli mpya zilizongezwa kwenye Toleo la 5, Mfumo wa Barua pepe (GMS) na mafunzo ya Sheria ya Serikali Mtandao, Mwongozo wa Matumizi Sahihi wa TEHAMA kwa watumiaji wakuu na wasimamizi wa Mfumo huu kama matarajio ya Serikali. Akitoa neno la Shukrani mmoja wa washiriki wa mafunzo Bw. George Jeriko Jombe ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kwa namna wanavyosimamia mifumo ya TEHAMA ya Serikali. Pia ametoa pongezi kwa Chuo Kikuu Mzumbe kwa kupata nafasi ya kuratibu na kufanikisha mafunzo hayo. Karibu Chuo Kikuu Mzumbe, “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu”