Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Ndaki ya Dar es Salaam, wamesisitiza dhamira yao ya kusaidia jamii kwa kutoa shauri za kitaaluma zinazolenga kuboresha maendeleo ya jamii na sekta mbalimbali. Haya yalibainika katika mafunzo ya uandishi wa ushauri za kitaaluma yaliyofanyika 21 Machi 2025, katika Ndaki hiyo jijini Dar es Salaam. Akizungumza wakati wa warsha hiyo Rasi wa Chuo Kikuu mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam Prof. Cyriacus Binamungu alisema miongoni wa majukumu ya Chuo Kikuu Mzumbe ni kufundisha, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalamu na aliwataka wafanyakazi hao kufatilia kwa makini mada zitakazo wasilishwa ili kuwajengea weledi katika majukumu yao ikiwemo kutoa ushauri wa kitaalamu kwa taasisi mbalimbali na Jamii. “Mafunzo haya ni muhimu katika kuwajengea uwezo wafanyakazi wetu hasa wanataaluma ili kuboresha ufanisi wa kazi zao na kutoa mchango wa kipekee kwa kuandaa na kutekeleza ushauri za kitaaluma katika nyanja mbalimbali za taaluma kama ilivyoelekezwa katika Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Chuo Kikuu Mzumbe”, Alisistiza Prof. Binamungu. Naye, Dkt. Mushumbusi Kato, ambaye aliwasilisha mada kuhusu uandaaji wa Ushauri wa Kitaaluma alieleza kuwa uandishi wa shauri za kitaaluma ni nyenzo muhimu katika kutoa suluhu za kitaalamu kwa changamoto zinazoukumba taasisi umma, binafsi na jamii kwa ujumla na kusisitiza kwamba wanataaluma wa Mzumbe wana jukumu kubwa la kutumia ujuzi wao katika kuboresha maisha ya watu, kutoa ushauri wa kitaaluma katika sekta mbalimbali, na kusaidia katika kuleta mabadiliko chanya katika jamii. "Uandishi wa shauri za kitaaluma ni njia mojawapo ya kuonyesha mchango wa taasisi ya elimu katika taasisi mbalimbali na jamii kupitia ushauri za kitaalamu kutoka kwa watalaamu wetu ,tunatoa suluhu za kisayansi na kitaaluma kwa changamoto zinazozikumba jamii yetu na kuimarisha maendeleo katika nyanja za elimu, afya, biashara,uongozi,uchumi, uhasibu,, manunuzi na mazingira na nyingine nyingi," alisema Dkt. Kato. Aidha Dkt. Edward Makoye na Bw. Elias Madafu kutoka Chuo Kikuu Mzumbe walisilisha mada kuhusu mbinu mbalimbali za kuandaa kozi fupi pamoja kuwapitisha katika sheria mbalimbali na miongozo ya kuandaa ushari za kitaalamu na kozi fupi kutoka Chuo Kikuu Mzumbe na pamoja na sheria mpya za manunuzi. Akifunga warsha hiyo, Mratibu warsha hiyo, kutoka Kurugenzi ya Huduma za Jamii Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Bertha Mwinuka alisema warsha hiyo imelenga kuwajengea wafanyakazi waendeshaji na wanataaluma wa Ndaki ya Dar es Salaam ueledi wa kuandaa na kutekeleza shauri za kitaaluma ambazo zitakuwa na manufaa kwa jamii na taasisi mbalimbali. Akiongea kwa niaba ya washiriki hao, Mkuu wa Kitengo cha Kozi fupi , Ubunifu na Ushauri za Kitaalaamu Dkt. Darlene Mutalemwa aliwashukuru waandaaji wa warsha hiyo kwani mada zilizowasilishwa zitawasaidia wafanyakazi hao kuboresha uwezo wao katika kutoa mchango wa kitaaluma kwa ajili ya maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla. “Tujifunze kwa Maendeleo ya watu”