News-Details

News >Details

RAIS SAMIA AAHIDI KUUNGA MKONO JITIHADA ZA MAENDELEO CHUO KIKUU MZUMBE

RAIS SAMIA AAHIDI KUUNGA MKONO JITIHADA ZA MAENDELEO CHUO KIKUU MZUMBE

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan,ameahidi kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Menejimenti ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kukiendeleza chuo hicho kwa kutumia fedha za makusanyo ya ndani kuanzisha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa majengo mapya na upanuzi wa kampasi zake ili kuboresha miundombinu ya kufundishia. Ametoa ahadi hiyo tarehe 04. 08. 2024 wakati wa Hafla ya Uwekaji wa jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa chuo hicho eneo la Maekani Kampasi Kuu Morogoro. Mhe. Rais amekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuendelea kuwa mahali sahihi pa kuandaa wasomi wanaoisaidia serikali na Taifa katika nyanja mbalimbali ikiwemo kijamii, siasa, Uchumi na Elimu. Aidha, amevutiwa zaidi na jitihada za chuo hicho kilichoanza utekelezaji wa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya ekari 980 zilizopo Kampasi kuu Morogoro ambao uliwasilishwa na Makamu Mkuu wa Chuo hicho Prof. William Mwegoha kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. “Niupongeze sana uongozi wa Chuo kwa kutumia vyanzo vya fedha za ndani kuanza kufanya kazi hii, nimefurahishwa sana na hilo, lakini mbali na fedha hizo tutaendelea kuleta fedha kupita vyanzo vingine kama vile Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) na vyanzo vingine”. Alisema Mhe. Rais. Mpango wa matumizi ya ardhi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe unahushisha ujenzi wa Kumbi za mihadhara, Maabara za TEHAMA, Makitaba za kisasa, Ofisi ya Vitizo na Skuli, Hospitali, Viwanja vya michezo, Makazi ya wanafunzi (Hosteli), Nyumba za wafanyakazi, Pamoja na miundombinu ya maji safi na maji taka.

None