Ikiwa ni katika utekelezaji wa jukumu mojawapo la wanataaluma wa Chuo Kikuu Mzumbe ambalo ni Kutoa Ushauri Kitaaluma, Kurugenzi ya Huduma za Jamii imeandaa na kuendesha warsha ya siku mbili ya ujuzi katika utoaji ushauri upande wa wanataaluma. Warsha hii ya siku mbili imeanza kutolewa kwa wanataaluma wa Ndaki ya Mbeya kuanzia tarehe 17, Machi 2025 katika Ukumbi wa Maktaba wa Ndaki hiyo. Warsha hii inalenga kutoa mafunzo ya umuhimu wa utoaji huduma za ushauri wa kitaalamu, kutoa ujuzi wa kujijengea uwezo na namna bora ya uandaaaji wa mapendekezo ya ushauri wa kitaalamu. Akifungua warsha hiyo, Bw. John Jorojik, Mkuu wa Idara ya Sayansi Jamii na Insia amewakaribisha washiriki kwa kutoa utangulizi mfupi kuhusu warsha hiyo, malengo na maadhimio huku akiwataka wawe makini na wenye kutoa ushirikiano ili waweze kuelewa lengo na umuhimu wa warsha hiyo katika utekelezaji wa majukumu yao. “Niwapongeze nyote kwa kuhudhuria warsha hii muhimu, kuweni huru hapa tupo kwa ajili ya kujifunza na kujengeana uwezo ili sote tuweze kuwa watoa ushauri mahiri katika maeneo yetu”, Alisema Bw. Jorojik. Akizungumza katika warsha hiyo, Dkt. Paul Kato ambaye ni Mwezeshaji wa warsha amewaeleza Wanataaluma juu ya umuhimu wa kutoa huduma za ushauri. “Ili kuweza kutatua tatizo la shirika au taasisi fulani, kukuza na kutambua fursa mpya lazima kuwepo na mtoa ushauri wa kitaalamu, ndio maana tupo hapa kuwajengea ujuzi na uwezo ili basi nafasi zinapotokea ya kutoa ushauri wanataaluma wa Mzumbe wawe ni kipaumbele katika nafasi hizo”. Dkt. Kato. Warsha hii inadhihirisha wazi jitihada za Chuo Kikuu Mzumbe za kuwajengea ufanisi na uwezo wanataaluma ili kuongeza chachu ya maendeleo binafsi ya wanataaluma, Chuo na jamii yote inayotuzunguka. Hivyo basi, Chuo Kikuu Mzumbe kinawakaribisha wadau wetu wote wenye uhitaji wa huduma za Ushauri wa Kitaalamu kutumia wanataaluma wetu wenye uwezo, ujuzi, maarifa na umahiri wa kutoa ushauri bora katika maeneo mbalimbali kama vile kutatua changamoto, kuandaa mipango mikakati ya muda mfupi na mrefu, kuongeza ujuzi na kuibua fursa mpya. #tujifunzekwamaendeleoyawatu