Chuo Kikuu Mzumbe, kupitia Skuli ya Biashara, kimeandaa mafunzo maalumu kuhusu Huduma kwa Wateja na Usimamizi wa Utoaji wa Huduma Bora, yaliyofanyika tarehe 26 Machi 2025 Kampasi Kuu Morogoro. Mafunzo haya yamewaleta pamoja washiriki kutoka sekta mbalimbali kwa lengo la kuboresha ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wateja na kujenga mahusiano bora kati ya taasisi na wateja wake. Yamehusisha Wafanyakazi wa Chuo Kikuu Mzumbe, Wafanyakazi wa CRDB na NMB Benki zilizopo Chuo Kikuu Mzumbe, Wahudumu wa Mikahawa, Mama Lishe na watoa huduma wanaozunguka Chuo Kikuu Mzumbe. Akifungua mafunzo hayo, Amidi wa Skuli ya Biashara, Dkt. Gabriel Vitus Komba, alisisitiza umuhimu wa huduma bora kwa maendeleo ya taasisi yoyote. “Huduma kwa wateja ni nguzo muhimu katika mafanikio ya biashara na taasisi za umma. Uboreshaji wa huduma unahitaji kujifunza mbinu bora na kujenga utamaduni wa kuwajali wateja katika kila hatua ya utoaji wa huduma,” alisema Dkt. Komba. Mafunzo haya yalihusisha mada mbalimbali zilizoongozwa na wataalamu wa sekta ya masoko, ujasiriamali na huduma kwa wateja. Prof. Hawa Petro Tundui alieleza kuhusu aina za wateja na jinsi ya kuwahudumia kwa ufanisi, huku Mr. Robinson Samwely akifafanua dhana ya Usimamizi wa Mahusiano na Wateja (CRM). Mr. Lwako Lubida alieleza changamoto na mbinu za kuboresha utoaji wa huduma bora, huku Mr. Miraji Mohamed Hussein akieleza mikakati ya marekebisho ya huduma pale inaposhindikana. Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Masoko na Ujasiriamali, Dkt. Robert Makorere, aliwahimiza washiriki kutumia maarifa waliyojifunza kuboresha huduma kwa wateja katika maeneo yao ya kazi. “Ubora wa huduma unapaswa kuwa sehemu ya utamaduni wa kila taasisi. Mafunzo haya ni mwanzo wa safari ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja ili kuleta maendeleo chanya kwa taasisi na jamii kwa ujumla,” alisema Dkt. Makorere. Mafunzo haya yametajwa kuwa hatua muhimu katika kuinua viwango vya utoaji wa huduma kwa wateja, huku washiriki wakiahidi kutekeleza mbinu walizojifunza katika kazi zao za kila siku.