News-Details

News >Details

WADAU WA MAZINGIRA NA UJASIRIAMALI WAKUTANA CLIMATHON MOROGORO

WADAU WA MAZINGIRA NA UJASIRIAMALI WAKUTANA CLIMATHON MOROGORO

Katika jitihada za kutafuta suluhisho bunifu kwa changamoto za tabianchi, wadau wa mazingira, wajasiriamali na wataalamu wa sekta mbalimbali wamekutana katika Jukwaa la Ubunifu wa suluhisho endelevu kwa changamoto za Tabianchi (CLIMATHON) ambalo linawezesha vijana kubuni na kuendeleza mawazo kwa maendeleo endelevu. Tukio hilo limekuwa fursa kwa wabunifu chipukizi kubuni suluhisho kwa changamoto za kilimo na usimamizi wa taka, huku likiwapa washiriki nafasi ya kushirikiana na kuendeleza miradi kwa vitendo. Mafunzo hayo yalifunguliwa rasmi na Prof. Emmanuel Chao, Meneja wa Ubunifu, Ujasiriamali na Ushirikiano wa Kitasnia Chuo Kikuu Mzumbe, ambaye amesisitiza umuhimu wa ubunifu na ushirikiano wa wadau katika kutatua changamoto za mazingira. Akizungumza na washiriki, Prof. Chao amesema kuwa changamoto za tabianchi zinahitaji suluhisho bunifu na jumuishi, huku akibainisha kuwa kupitia Climathon, vijana wanapata nafasi ya kufikiria kwa upana, kushirikiana na kubuni miradi inayoweza kubadili maisha na kulinda mazingira. Awali, washiriki walipokelewa rasmi na Inés Mas de la Peña, ambaye alieleza kuwa jukwaa hilo ni fursa muhimu kwa vijana na wadau wa mazingira kuja na suluhisho endelevu yanayojikita katika ubunifu na ujasiriamali. Alisema kuwa Climathon ni sehemu sahihi ya kuleta mabadiliko hayo. Watoa mada mbalimbali pia walichambua changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi, hasa katika sekta ya kilimo na usimamizi wa taka. Bw. Otaigo Elisha, mtaalamu wa kilimo, alieleza jinsi mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri uzalishaji wa chakula, huku akisisitiza hitaji la kutumia teknolojia rafiki kwa mazingira. Kwa upande wake, Bw. Emmanuel Makero, mtaalamu wa usimamizi wa taka, alieleza namna taka zisipodhibitiwa zinavyoweza kuchangia ongezeko la joto duniani. Mbali na mijadala hiyo, washiriki walipata mafunzo ya uandaaji wa miradi na mbinu za kuwasilisha mawazo ya biashara, ambapo Dkt. Irene Isibika aliongoza mafunzo hayo ili kuwawezesha washiriki kuwasilisha kwa ufanisi mawazo yao kwa wawekezaji na wadau wengine muhimu. Pia, washiriki walipata fursa ya kuboresha mawazo yao kwa kutumia Climate Model Canvas, na kuwasilisha miradi yao mbele ya jopo la majaji ambapo washindi walitangazwa na kupatiwa vyeti kama sehemu ya kuthamini mchango wao katika kutengeneza suluhisho la changamoto za mazingira. Tukio hilo limeendelea kuthibitisha kuwa Climathon Morogoro ni jukwaa muhimu kwa vijana na wadau wa mazingira kuungana, kushirikiana, na kubuni mbinu mpya za kukabiliana na changamoto zinazohusiana na tabianchi, huku likichochea uvumbuzi na ujasiriamali miongoni mwa vijana.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None