Chuo Kikuu Mzumbe ni Taasisi ya umma ambayo ilianzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Chuo Kikuu Mzumbe Na. 21 ya mwaka 2001. Sheria hiyo ilifutwa na Sheria ya Vyuo Vikuu Na. 7 ya mwaka 2005 ambayo inasimamia masuala yote yanayohusu Elimu ya vyuo Kikuu nchini Tanzania. Kwa sasa, Chuo kinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Hati Idhini ya Chuo Kikuu Mzumbe, 2007 iliyotolewa chini ya Kifungu Na. 25 cha Sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005. Chuo kimeendelea kukua kwa kasi ambapo hadi sasa kina jumla ya Wanafunzi 16,462 kutoka Kampasi kuu -Morogoro, Ndaki ya Mbeya pamoja na ndaki ya Dar es Salaam (Kampasi kuu 11,284, Mbeya 3,385 na Dar es Salaam 1793). Kati ya hao, wanafunzi 8356 sawa na asilimia 51 ni wanaume, na wanafunzi 8,106 sawa na asilimia 49 ni wanawake. Chuo kina matawi matatu, yaani, Kampasi Kuu iliyopo Morogoro, Kampasi ya Dar es Salaam, Kampasi ya Mbeya na kinaendelea na ujenzi wa Kampasi mpya ya Tanga inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (Higher Education for Economic Transformation-HEET). Majukumu makubwa ya Chuo Kikuu Mzumbe ni kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kufanya utafiti, kutoa ushauri wa kitaalam na kutoa huduma kwa jamii. Chuo Kikuu Mzumbe kinaendesha programu 77 za masomo katika fani mbalimbali na kwa ngazi tofauti zikiwemo Astashahada (8), Stashahada (7), Shahada za Kwanza (30), Shahada za Umahiri (26) na Shahada za Uzamivu (“PhD”) katika maeneo yote ya ubobezi yanayotolewa Chuo Kikuu Mzumbe. Chuo Kikuu Mzumbe kimejijengea umahiri na ubobevu kwa miaka mingi katika fani za Utawala wa Umma, Menejimenti ya Rasilimali Watu, Serikali za Mitaa, Mifumo ya Afya na Mazingira, Ufuatiliaji na Tathmini Katika Afya. Chuo Kikuu Mzumbe pia kimebobea katika Uongozi wa Biashara, Ujasiriamali na Ubunifu; Uhasibu na Fedha, Ununuzi na Ugavi, Uchumi ikiwa ni pamoja na Mipango na Sera, Mipango na Menejimenti ya Miradi na Maendeleo ya Watu, Sheria, Elimu (Hisabati na Lugha, Biashara na Uhasibu), Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Menejimenti ya Mifumo, Menejimenti ya Habari na Mawasiliano), Sera za Umma, Menejimenti ya Uhandisi wa Viwanda na Menejimenti ya Uzalishaji na Usimamizi. Chuo Kikuu Mzumbe kimeendelea kuwa Taasisi bora ya elimu ya juu nchini Tanzania, kikijivunia historia yake ndefu ya kutoa wataalamu na viongozi mahiri kwenye nyanja mbalimbali. Kati ya viongozi wengi waliosoma na Chuo Kikuu Mzumbe kwenye masuala ya uongozi na kufanikiwa kushika nafasi za juu katika uongozi ni pamoja na Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Jumuiya ya Chuo Kikuu Mzumbe inayo kila sababu ya kuona fahari na kujivunia mafanikio lukuki yaliyopatikana katika kipindi cha utawala wake kwani umahiri aliouonesha kama kiongozi mkuu na uzalendo wake kwa nchi ni uthibitisho wa kutosha kudhihirisha kuwa yeye ni mmoja wa wahitimu bora wa Utawala wa Umma waliosoma katika Chuo hiki. Katika kipindi kifupi cha uongozi wake wa miaka minne, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameliwezesha taifa la Tanzania kupiga hatua kubwa kwenye nyanja zote za maendeleo nchini ikiwemo uboreshwaji wa miundombinu, huduma za jamii na uchumi lakini kubwa zaidi ambalo makala hii itaangazia ni mapinduzi makubwa kwenye sekta ya elimu na kwa namna ya kipekee Chuo Kikuu Mzumbe kilivyonufaika na Uongozi wake ambao umekuwa chachu ya mabadiliko makubwa, hususan kwenye ubora wa elimu ya juu, utafiti, ushirikiano wa kimataifa, na kuboresha mazingira ya kujifunza. i. Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi(HEET) ni juhudi za Serikali ya Tanzania, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, za kuboresha sekta ya elimu ya juu ili kuchangia katika mageuzi ya kiuchumi ya nchini. Mradi huu unatekelezwa kwa mkopo wa Benki ya Dunia na umelenga kuboresha miundombinu ya elimu ya juu, kuongeza fursa za udahili, na kuhamasisha ubunifu miongoni mwa wanafunzi. Chuo Kikuu Mzumbe ni moja kati ya Taasisi za Elimu ya Juu ambazo zimenufaika na mradi huo kwa kupatiwa kiasi cha dola milioni 21 za kimarekani (takribani shilingi za kitanzania bilioni 50) kwa lengo la kuimarisha miundombinu ya kujifunza na kufundishia pamoja na kuanzisha kampasi mpya mkoani Tanga. Tangu kuanza kwa mradi huo mwaka 2021 Chuo Kikuu Mzumbe kimepiga hatua kwenye utekelezaji wa mradi huo ambapo kwa sasa kinaendelea na ujenzi wa majengo ya kisasa ya taaluma na kituo cha TEHAMA katika kampasi kuu na kampasi ya Tanga. Aidha ili kuendana na malengo ya mradi wa HEET ya kuzalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika sokoni ambao watakuwa na uwezo wa kuchagiza uchumi na kuchangia maendeleo endelevu ya taifa, Chuo kimefanya mapitio ya mitaala kwa programu za shahada za awali pamoja na kuanzisha programu mpya. Jumla ya programu 10 ziko katika hatua za mapitio na programu 11 mpya ziko katika hatua mbalimbali za mchakato wa kuanzishwa. Hadi sasa jumla ya programu 20 zimewasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya maombi ya kupatiwa ithibati. Kadhalika kwa upande wa programu za shahada za umahiri Chuo kimeendelea kuchukua hatua za kimkakati kuboresha mitaala yake pamoja na kuanzisha programu za kimkakati. Baadhi ya programu zinazotarajiwa kuanzishwa ni pamoja na Master of Implementation Science (MIS), Master of Digital Finance, Master of Law in ICT Law, Master of Development Monitoring & Evaluation (MDME), na Master of Arts in Kiswahili (MAK). Kupitia mradi wa HEET Chuo pia kimeanza usanifu wa miundombinu ya maktaba ya kidijitali na mtandao (digital and virtual library infrastructure). Aidha kimeweza kutengeneza studio (multimedia) yenye vifaa vya kisasa kwa ajili ya kusaidia ufundishaji wa masomo kwa njia ya mtandao (Blended Learning) na kimeweza kununua samani za kituo cha msaada kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum, vikiwemo kompyuta, vifaa vya teknolojia saidizi (Assistive and adaptive technologies) na vitabu vya maktaba n.k. Thamani ya jumla ya vifaa vyote hivyo ni Shilingi za kitanzania takribani bilioni 2.4. Inategemewa kwamba kukamilika kwa miundombinu itakayojengwa kupitia mradi wa HEET,idadi ya wanafunzi itaongezeka kutoka 16,462 waliopo sasa hadi takribani wanafunzi 17,000 mwaka 2026/27. Benki ya Dunia imeonyesha kuridhishwa na hatua za utekelezaji wa mradi huu kwa Chuo Kikuu Mzumbe kwani hivi karibuni ujumbe ulioambatana na ujumbe kutoka wizara ya Elimu,Sayansi na ulitembelea na kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo ambapo waliridhika na kuipongeza Menejimenti ya Chuo kwa kusimamia vyema mradi huo. ii. Mikopo ya Elimu ya juu Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wamekuwa wanufaika wakubwa wa mikopo ya elimu ya juu ambapo idadi yao imeendelea kuongezeka kutoka 7,434 mwaka 2022 hadi kufikia 10,454 mwaka 2025. kiasi cha zaidi ya TZS.32,133,784,816.00 kilitolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kulipia gharama za malazi, chakula, masomo n.k . Ongezeko hilo linafanya jumla ya wanafunzi 3,109 kunufaika zaidi na mikopo ya Elimu ya Juu kati mwaka 2022 hadi 2025 miongoni mwao kwa mwaka 2024/2025 wanawake wakiwa 5,000 (sawa na 48%) na wanaume 5,464 (sawa na 52% ) ukilinganisha kwa mwaka 2021/2022 wanawake wakiwa 3,170 sawa (43%) na wanaume 4,175 sawa na (57%) . Kuongezeka kwa idadi ya wanufaika wa mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu kumechochea vijana wengi kujiunga na Elimu ya Juu na kuongeza udahili kwa Chuo kikuu Mzumbe ikiwa ni pamoja na wale wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini na hivyo kukifanya Chuo hiki kuwa miongoni mwa Taasisi muhimu zinazozalisha wataalamu wa ngazi mbalimbali wenye ujuzi na maarifa kwa ajili ya kujenga uchumi wa nchi yetu. iii. Kuongezeka kwa Ajira, kupanda madaraja na kulipwa malimbikizo ya Watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, Chuo Kikuu Mzumbe kimefanikiwa kuongeza ajira kutoka watumishi 615 mwaka 2021 hadi 840 mwaka 2025 kati yao wahadhiri ni 432 na waendeshaji ni 408 na hivyo kupelekea kutatua changamoto ya upungufu wa watumishi iliyokuwa ikikikabili Chuo kwa muda mrefu. Aidha watumishi takribani 347 wameweza kupanda madaraja tangu mwaka 2021. Kadhalika Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan imeweza kulipa kiasi cha shilingi 721,071,851.32 ikiwa ni malimbikizo ya madeni ya Watumishi wa Chuo Kikuu Mzumbe waliyokuwa wakiidai Serikali kwa muda mrefu. Uboreshaji wa Miundombinu na Mazingira ya Kujifunzia kwa fedha za ndani i. Ujenzi wa mabweni ya wanafunzi kampasi kuu na Ndaki ya Mbeya Chuo Kikuu Mzumbe kwa kutambua uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto za ubora wa miundombinu ya elimu, Chuo kiliamua kuunga mkono juhudi za Serikali. Kupitia mapato ya ndani Chuo kimefanikiwa kuongeza miundombinu muhimu, ikiwemo ujenzi wa hosteli 4 kampasi kuu, zilizokamilika mwaka 2023 kwa gharama ya shilingi bilioni 6.7. Majengo haya mapya yameweza kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto ya malazi.Wanafunzi zaidi ya 1,0026 wameweza kupata nafasi za malazi na hivyo kuboresha hali ya maisha na masomo kwa wanafunzi. Aidha Chuo kimeanzisha mradi kujenga hosteli ya wanafunzi wa kike katika Ndaki ya Mbeya ambayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya malazi. Changamoto hiyo iliifanya Menejimenti ya Chuo kubuni mradi wa ujenzi wa hosteli yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 800 mradi ambao unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 5.8. Hadi sasa jumla ya shilingi milioni 90.2 zimeshakusanywa. Serikali kupitia Wizara ya Elimu imeona umuhimu wa kuunga mkono mradi huu, na Chuo kinatarajia kupatiwa fedha toka serikalini ili kuongea nguvu katika kutelekeza mradi huo. ii. Ujenzi wa jengo la Utawala na uboreshaji wa barabara za ndani Chuo kinakamilisha ujenzi wa Jengo la Utawala katika Kampasi Kuu, mradi wenye thamani ya takriban shilingi bilioni 4.8 ambao umelenga kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wanafunzi, hivyo kuongeza ufanisi wa utendaji na kuboresha ubora wa elimu inayotolewa. Ujenzi wa jengo hili umefikia asilimia 94 na kukamilika kwake kutaongeza tija kwa Watumishi wa Chuo. Kadhalika Chuo kimeendelea kuboresha miundombinu ya barabara za ndani ya Chuo kampasi kuu kwa kujenga barabara za kiwango cha zege zenye urefu wa mita 1,510 pamoja na kufanya marekebisho katika maeneo ya lami yaliyoharibika. Mradi huu umefikia asilimia 90 ya utekelezaji na utagharimu takriban Tshs. 924,000,000.00 hadi kukamilika kwake. iii. Ujenzi wa zahanati Kampasi ya Mbeya na uboreshaji wa kituo cha afya Kampasi Kuu Ili kuhakikisha Wanafunzi wanakuwa na uhakika wa afya zao wakati wote wanapoendelea na masomo, Chuo kimeendelea kuimarisha huduma za afya ikiwemo ukamilishaji wa ujenzi wa zahanati katika Ndaki ya Mbeya ambao umegharimu jumla ya shilingi milioni 465.7 na sasa zahanati hii inatoa huduma za afya kwa wanajumuiya ya Chuo Kikuu Mzumbe na jamii inayozunguka Chuo. Aidha, Chuo kinakamilisha ujenzi wa jengo la upasuaji katika kituo cha Afya cha Kampasi kuu kwa thamani ya shilingi millioni 133.05 ambao kwa sasa umefikia asilimia 90. Hivyo, wanafunzi watanufaika moja kwa moja na huduma bora na za haraka za afya ndani ya Chuo na hatua hiyo itawapa nafasi ya kujikita zaidi kwenye masomo yao na kuboresha ustawi wao wa kitaaluma wawapo chuoni. iv. Kuanzishwa kwa kituo cha Tegeta kwa masomo ya shahada za awali Ndaki ya Dar es Salaam Chuo Kikuu Mzumbe kimefanikiwa kupanua Ndaki yake ya Dar es Salaam ambayo hapo awali ilikuwa ikitoa masomo ya uzamili pekee katika eneo la Upanga. Mwaka 2021 kwa mara ya kwanza Chuo Kikuu Mzumbe kilianzisha kituo kipya cha Tegeta kwa ajili ya masomo ya Shahada za awali ambapo jumla ya Wanafunzi 155 walidahiliwa katika mwaka huo, ambapo wanafunzi 126 walifanikiwa kuhitimu masomo yao katika mahafali ya 22 ya mwaka 2023. Hadi sasa kituo cha Tegeta kina jumla ya Wanafunzi 758 na kinaendelea kutoa huduma ya masomo kwa kozi za Shahada ya Uhasibu na Fedha-Sekta ya Biashara (Bachelor of Accounting and Finance Business Sector-BAF – BS) na Shahada ya Utawala wa Umma (Bachelor of Public Administration (BPA). v. Kuongezeka kwa miradi ya utafiti na machapisho ya kitaaluma Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Dkt.Samia, Chuo Kikuu Mzumbe kimefanikiwa kuandika na kushinda miradi ya tafiti ambayo imelenga kutatua changamoto mbalimbali nchini na kuhudumia jamii. Chuo kimeshiriki kwenye tafiti za maendeleo ya jamii, mazingira, utawala, afya, uchumi, teknolojia, sheria, uhasibu na menejimenti. Miradi yote hiyo ya tafiti imeweza kuliingizia taifa takribani kiasi cha dola za kimarekanai Milioni 8.6. Aidha Chuo kimeweza kuonekana kwenye majukwaa ya kitaaluma ya kimataifa kutokana na machapisho mbalimbali yaliyochapishwa na wanataaluma wake. Zaidi ya machapisho 383 yametolewa kwenye majarida mbalimbali yakiwemo ya ndaniya nchi na ya kimataifa kama vile Scientific Reports (Nature), PloS, Health Science Reports, Scientific African, Women Studies International Forum (Elsevier Science) Chuo Kikuu Mzumbe kinavyojivunia uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Chuo Kikuu Mzumbe kinafahamika zaidi kwa ubobezi wake wa kuzalisha viongozi wenye uwezo wa kushughulikia changamoto za kijamii. Rais Dkt. Samia akiwa ni zao la Chuo Kikuu Mzumbe, ameonyesha uongozi wa kipekee unaozingatia ushirikishwaji wa wananchi katika maamuzi ya maendeleo. Maamuzi yake yanayozingatia ushahidi yanaendana na msingi wa taaluma ya Chuo Kikuu Mzumbe, ambayo inahimiza matumizi ya utafiti na uchambuzi wa kina katika maamuzi ya kiutawala na kijamii. Kupitia falsafa yake ya 4R, Rais Samia ameonyesha mfano bora wa kutumia maarifa na utafiti katika kukuza utulivu na maendeleo ya kitaifa. Rais Samia ameleta mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi, akisisitiza utawala bora na uwajibikaji, mambo ambayo Chuo Kikuu Mzumbe kinayahimiza kwa wahitimu wake. Tarehe 24 Novemba, 2024 Chuo Kikuu Mzumbe kilimtunuku Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan Shahada ya Udaktari wa Heshima katika Uongozi. Maamuzi ya kumtunuku Mheshimiwa Rais heshima hiyo yalizingatia kuwa Chuo kimejikita katika kukuza uongozi bora, uvumbuzi, na maadili katika utumishi wa umma, maadili ambayo Rais Samia ameyaonyesha kwa dhahiri kupitia safari yake ya uongozi na mchango wake kwa taifa. Katika hotuba yake ya kupokea shahada hiyo, Mhe. Rais alionesha kufurahishwa na kazi inayofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe, hususan kubuni na kutelekeza miradi kadhaa ya miundombinu kwa kutumia fedha za ndani na kuahidi ushirikiano toka serikalini kwa kuanzia na mradi wa hosteli ya wasichana Ndaki ya Mbeya HITIMISHO: Maendeleo makubwa ya Chuo Kikuu Mzumbe yaliyopatikana ndani ya muda mfupi kwenye kipindi ambacho Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa madarakani ni uthibitisho tosha wa kazi kubwa inayofanywa na Rais wetu. Uongozi wake mahiri umeleta heshima kubwa kwa nchi yetu katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, Afrika na duniani kote. Hii imejidhirisha zaidi kwenye Diplomasia ya Uchumi ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa wawekezaji katika Sekta mbalimbali nchini kwetu. Tunampongeza sana Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza miaka minne akiwa madarakani kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo ameonesha umahiri wa hali ya juu katika kuongoza Watanzania na kusimamia rasilimali za nchi yetu kwa manufaa ya wananchi wote. Tunamwombea mafanikio makubwa katika kuliongoza Taifa letu ili kuleta maendeleo na mageuzi makubwa ya kijamii na kiuchumi. Sisi wana Jumuiya ya Chuo Kikuu Mzumbe tutaendelea kumuunga mkono kwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kuliletea taifa letu maendeleo pamoja na kuhudumia wananchi tukisimamia kauli mbiu yetu ya Chuo inayosema. “Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu”.
Maendeleo ya ujenzi wa jengo la TEHAMA na Ubunifu Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro eneo la Maekani, ambalo ujenzi wake unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Elimu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET Project)
Maendeleo ya ujenzi wa jengo la Taaluma Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro eneo la Maekani, ambalo ujenzi wake unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Elimu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET Project)
Maendeleo ya Ujenzi wa Nyumba za Wafanyakazi Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga, ambayo ujenzi wake unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET - Project)
Maendeleo ya Ujenzi wa Jengo la Utawala Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga, ambayo ujenzi wake unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET - Project)
Maendeleo ya Ujenzi wa Mkahawa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga, ambayo ujenzi wake unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET - Project)
Maendeleo ya Ujenzi wa Kituo cha Afya Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga, ambayo ujenzi wake unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET - Project)
Maendeleo ya Ujenzi wa Mabweni ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Tanga, ambayo ujenzi wake unatekelezwa kupitia fedha za Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET - Project)
Muonekano wa jengo jipya la Utawala la Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro Eneo la Maekani
Muonekano wa jengo jipya la Utawala la Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro Eneo la Maekani
Muonekano wa jengo jipya la Utawala la Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro Eneo la Maekani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hasan (kulia) akitunukiwa Shahada ya Udaktari wa heshima katika uongozi na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohammed Shein.