News-Details

News >Details

CHUO KIKUU MZUMBE CHASHIRIKI KIKAO KAZI CHA WARATIBU WA MRADI WA HEET NCHINI

CHUO KIKUU MZUMBE CHASHIRIKI KIKAO KAZI CHA WARATIBU WA MRADI WA HEET NCHINI

Chuo Kikuu Mzumbe kimeshiriki kikamilifu katika Kikao Kazi cha Utekelezaji wa Mradi wa HEET (Higher Education for Economic Transformation), kinachoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (MoEST) kwa kushirikiana na Benki ya Dunia. Kikao hiki kinalenga kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kupitia HEET katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu nchini Tanzania. Akifungua kikao kazi hicho kilichofanyika tarehe 2 Aprili 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Elimu ya Juu, Prof. Peter Msofe ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesisitiza umuhimu wa Mradi wa HEET katika kuleta mageuzi kwenye elimu ya juu nchini. "Mradi wa HEET ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuhakikisha vyuo vikuu vinakuwa na miundombinu bora, mitaala inayokidhi mahitaji ya soko la ajira, na ushirikiano wa karibu na sekta ya viwanda. Ni muhimu kwa taasisi zote zinazoshiriki kuhakikisha kuwa rasilimali zinazotolewa zinatumika kwa tija na ufanisi," alisisitiza Prof. Msofe Kwa upande wake, Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa HEET, Dkt. Kennedy Hosea, amepongeza juhudi za taasisi zote zinazotekeleza mradi huu na kusisitiza umuhimu wa mashirikiano kati ya vyuo vikuu kwa lengo la kubadilishana uzoefu na mbinu bora za usimamizi wa rasilimali. "Kikao hiki ni fursa muhimu kwa taasisi zetu za elimu ya juu kujifunza kutoka kwa wenzao, kushirikiana, na kuhakikisha kuwa tunafuata viwango vya kimataifa katika usimamizi wa elimu, utawala bora, usimamizi madhubuti wa rasilimali, na matumizi ya mifumo ya kidijitali ni mambo muhimu tunayopaswa kuzingatia ili kufanikisha HEET," alisema Dkt. Hosea. Aidha, katika kikao hicho kilihusisha mijadala juu ya usimamizi wa fedha, masuala ya mazingira na jamii, na maendeleo ya teknolojia ya kidijitali katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini. Ushiriki wa Chuo Kikuu Mzumbe katika kikao hiki unaonesha dhamira yake ya kuhakikisha Mradi wa HEET unatekelezwa kwa mafanikio na kuleta mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

None
None
None
None
None
None
None
None