Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway nchini Tanzania wametoa semina ya usawa kijinsia katika masuala ya uongozi na biashara kwa wanafunzi wa Chuo hicho ikiwa ni sehemu ya mpango mkakati wa Chuo wa kuwajengea uwezo wanafunzi ili waweze kuwa wabobezi katika nyanja mbalimbali na kufikia malengo yao. Akizungumza wakati akifungua Semina hiyo April 4, 2025, Naibu Rasi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam, Prof. Omary Swalehe amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya Mpango Mkakati wa Chuo Kikuu Mzumbe ya kuwakutanisha wanafunzi na wabobezi mbalimbali ili wawezi kuwasaidia kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao wawapo chuoni na baada ya kumaliza masomo yao. Naye, Balozi wa Norway nchini Tanzania, Mhe. Tone Tinnes amesema lengo la semina hiyo ni kutoa elimu ya usawa wa kijinsia katika uongozi na biashara ili kuhakikisha fursa sawa kwa wote na kuongeza kuwa uzoefu wa Norway unaonyesha kuwa uongozi unaoshirikisha jinsia unachochea ubunifu, ukuaji wa uchumi na biashara bora. Kwa upande wake Meneja wa Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Ushirikiano wa kitasnia Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Emmanuel Chao amesema semina hiyo ni matokea ya uhusiano mzuri wa chuo na taasisi nyingine ndani na nje ya nchi katika kuboresha elimu na kujenga uwezo wa masuala ya uongozi unaozingatia uwasa wa kijinsia mahali pa kazi pamoja na shughuli za kijamii katika taasisi za umma na sekta binafsi. Mafunzo yamegusa maeneo tofauti ikiwemo namna bora ya kuanzisha biashara pamoja na kutoa fursa kwa kuwapa nyenzo muhimu wanafunzi ili wanapomaliza chuo wajue wanafanya nini ili kufikia malengo na kuhisisitiza jamii umuhimu wa kuwa na utamaduni wa kujiendeleza kielimu pamoja na kujifunza kwa kutumia fursa ya mitandao ya kijamii jambo ambalo litasaidia kuongeza ufanisi katika utendaji. Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Imelda Lutebinga, amesema kuwa ni muhimu kuwapa elimu wanafunzi kwani ni sehemu ya kupanda mbegu, huku akieleza kuwa ATE imekuwa iendesha programu ya kuwajengea uwezo wanawake kulingana na uhitaji hasa katika nafasi ya uongozi na kwamba wameendelea kutoa programu ya kutoa elimu ya kujiami, kujieleza kwa ufasaha ili kuhakikisha wanawake wanakuwa na uwezo kuongeza katika nafasi yoyote ya uongozi. Naye, Mkurugenzi wa Tanzania Startup Association Bw. Zahoro Muhaji, amewataka wanafunzi kuwa wavumilivu, mawazo mazuri ya ujasiriamali pamoja na kutafuta mahusiano ya kibiashara kwa wawekezaji na watoa mitaji na wadau mbalimbali wakiwemo wanasheria ni mbinu muhimu kwani ni fursa ya kupata wawekezaji pamoja na wateja. Kwa upande wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Kituo Cha Tegeta wametoa shukrani kwa kupata mafunzo, kwani yamewasaidia kujifunza mbinu bora za kuanzisha na kuendesha biashara pamoja na uongozi ambazo zitawasaidia kuwa viongozi bora katika jamii na maeneo ya kazi. Watoa mada wametoka Taasisi za kibiashara nchini Norway (NHO), Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), pamoja na Taasisi ya Startup Association Tanzania ambapo wamesisitiza umuhimu wa wanafunzi kuwa na subira pamoja na kutengeneza mahusiano wadau ili kufikia fursa kwa haraka.