Chuo Kikuu Mzumbe kimezindua rasmi mradi wa AI4STEM, ambao unaolenga kuboresha elimu ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) kupitia matumizi ya Teknolojia ya Akili Unde (AI). Uzinduzi huu umefanyika tarehe 08 Machi 2025 katika Kampasi Kuu, Morogoro. AI4STEM — kifupi cha AI-Driven Inclusive STEM Learning in Tanzania — ni mradi unaotekelezwa na Chuo Kikuu Mzumbe - Tanzania na Chuo Kikuu cha Ghent cha nchini Ubelgiji. Mradi huu unalenga kuunganisha teknolojia za AI ili kuongeza ushirikishwaji na uhamasishaji katika elimu ya STEM kote Tanzania, hasa kwa wanafunzi wadogo. Mradi huu unatekelezwa chini ya Kitivo cha Sayansi na Teknolojia (FST), Idara ya Masomo ya Kompyuta, Chuo Kikuu Mzumbe na utatekelezwa kwa miaka mitano (2024 – 2029). Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha aliwapongeza waanzilishi wa mradi huo na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano huo. Alisema: “Hii ni hatua kubwa siyo tu kwa Chuo Kikuu Mzumbe bali pia kwa Taifa. Tunajivunia kuwa mstari wa mbele katika mradi unaoiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia katika matumizi ya Akili Unde katika elimu. Ninawahakikishia kuwa Uongozi wa Chuo uko tayari kutoa usaidizi katika utekelezaji wa mradi huu muhimu.” Awali, Mratibu wa Mradi ambaye pia ni Mhadhiri kutoka Idara ya Masomo ya Kompyuta, Dkt. Tupokigwe Isagah, alitoa muhtasari wa mradi wa AI4STEM, kisha alimkaribisha Prof. Tony Belpaeme kutoka Chuo Kikuu cha Ghent ambaye alieleza uzoefu kuhusu nafasi ya AI na roboti katika elimu ya watoto. Mambo mengine muhimu ni pamoja na maonesho ya roboti wa kijamii aliyebuniwa kama mfano wa kufundisha somo la hisabati, akioneshwa na Bw. Edger Lutatora na Bi. Elina Ntahomvukye, pamoja na mpango wa kuanzishwa kwa Kituo kipya cha Utafiti na Ubunifu katika Teknolojia ya Akili Unde uliowasilishwa na Mkuu wa Idara ya Masomo ya Kompyuta, Dkt. Eng. Morice Daudi. Kwa upande wake, Dkt. Irene Isibika aliwasilisha tathmini ya mahitaji, maonesho ya roboti, na mijadala ya mipango ya kimkakati, zikionesha dhamira ya mradi katika kutoa suluhisho la kielimu lenye matokeo ya moja kwa moja. Mradi wa AI4STEM haulengi tu katika kuingiza teknolojia madarasani, bali unalenga kuandaa njia jumuishi za kutatua changamoto za elimu nchini Tanzania. Kadri mradi utakavyoendelea kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, wadau wanatarajia kuona mabadiliko makubwa katika namna masomo ya STEM yanavyofundishwa na kujifunzwa, hivyo kuwaandaa vijana wa kizazi kijacho kwa ujuzi unaohitajika katika dunia ya kidijitali inayokua kwa kasi.