News-Details

News >Details

BW. KAVISHE AIBUKA KIDEDEA KUTETEA TASNIFU YAKE YA UZAMIVU CHUO KIKUU MZUMBE

BW. KAVISHE AIBUKA KIDEDEA KUTETEA TASNIFU YAKE YA UZAMIVU CHUO KIKUU MZUMBE

Bw. Wilfred Kavishe, mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Skuli ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe, ameandika historia kwa kutetea kwa mafanikio tasnifu yake ya utafiti leo tarehe 9 Aprili 2025, Kampasi Kuu, Morogoro. Utetezi huo ulifanyika mbele ya jopo la watahini lililoongizwa na Prof. Hawa Tundui. Mada ya tasnifu ya Bw. Kavishe inasema “Athari za Sifa za Maafisa wa Mikopo na Uelewa wao katika Uidhinishaji wa Mikopo Kupitia Uchangishaji Fedha wa Pamoja: Uchunguzi kwa Washirika wa Kiva”. Utafiti huu umechambua kwa kina jinsi sifa binafsi kama vile uzoefu, uadilifu na uelewa wa maafisa wa mikopo unavyoathiri mchakato wa kuidhinisha mikopo inayotolewa kwa njia ya kuchangia kwa pamoja kupitia majukwaa ya kidijitali kama Kiva. Akiwasilisha matokeo yake, Bw. Kavishe alieleza kuwa maafisa wa mikopo wenye uelewa mkubwa na maadili ya kazi huchangia kwa kiasi kikubwa kuongeza ufanisi na usawa katika mchakato wa utoaji mikopo. “Ni muhimu taasisi za kifedha kuwekeza katika kuwajengea uwezo maafisa wake, kwani wao ndio kiungo muhimu kati ya watoa huduma na walengwa wa mikopo,” alisisitiza. Katika mapendekezo yake, ameshauri kuwepo kwa miongozo thabiti ya maadili, mafunzo ya mara kwa mara na matumizi sahihi ya teknolojia ili kuhakikisha uamuzi wa utoaji mikopo unakuwa wa haki na unaolenga kusaidia walengwa kwa tija. Baada ya majadiliano ya kina, Mwenyekiti wa jopo la watahini, Prof. Hawa Tundui, alieleza kuridhishwa na namna Kavishe alivyoonesha umahiri wa hali ya juu katika kuwasilisha hoja zake, na kusisitiza kuwa utafiti wake una mchango mkubwa katika kuboresha mifumo ya fedha jumuishi nchini. Utetezi huo umeendelea kuonyesha kuwa Chuo Kikuu Mzumbe si tu taasisi ya elimu ya juu, bali ni kitovu cha mawazo bunifu na tafiti zenye kuleta mabadiliko katika jamii. Chuo Kikuu Mzumbe – Tujifunze kwa Maendeleo ya Watu.

None
None
None
None
None
None
None
None
None