Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kitivo cha Sayansi na Teknolojia, Idara ya Masomo ya Kompyuta, kimeendesha Mhadhara wa Umma uliojikita katika mada ya "Kushamiri kwa Teknolojia ya Akili Unde na Namna Inavyoathiri Maisha ya Kila Siku". Mhadhara huo umefanyika tarehe 09 Aprili 2025, chini ya uratibu wa Mradi wa AI4STEM (AI-Driven Inclusive STEM Learning in Tanzania). Akizungumza katika ufunguzi wa mhadhara huo, Mtiva wa Kitivo cha Sayansi na Teknolojia, Dkt. Joseph Sungau, alieleza kuwa lengo kuu ni kutoa uelewa mpana kwa wanafunzi na wafanyakazi wa Mzumbe kuhusu matumizi chanya ya teknolojia hiyo ya kisasa katika maisha ya kila siku. Pia, alisisitiza juu ya umuhimu wa kuwa na maarifa sahihi kuhusu Akili Unde(AI) ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia duniani. Kwa upande wake mtoa mada mkuu, Prof. Tony Belpaeme kutoka Chuo Kikuu cha Ghent nchini Ubelgiji ambaye ni Profesa wa Roboti na Mifumo ya Kifahamu (Professor in Robotics and Cognitive Systems), alifafanua kwa kina kuhusu kushamiri kwa Teknolojia ya Akili Unde: Namna Inavyoathiri Maisha ya Kila Siku. Katika maelezo yake, Prof. Belpaeme alisisitiza juu ya nafasi ya Akili Unde na roboti katika kuleta mapinduzi kwenye sekta ya elimu, afya na huduma mbalimbali za kijamii, sambamba na changamoto zinazoweza kujitokeza endapo matumizi ya teknolojia hiyo hayatadhibitiwa ipasavyo. Mhadhara huo ulihusisha pia majadiliano ya wanajopo kutoka maeneo mbalimbali ya kibobezi waliotoa michango yao, akiwemo Dkt. Lorah Bosoline Madete kutoka Tume ya Mipango, Bw. Melchiory Baltazary kutoka TAMISEMI, Dkt. Tupokigwe Isagah na Dkt. Morice Daud ambao ni Wahadhiri wa Masomo ya Kompyuta Chuo Kikuu Mzumbe. Mjadala huo uliendeshwa na Mratibu wa Mradi, Bw. Edger Lutatora. Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi walieleza kufurahishwa na elimu waliyoipata, wakisema kuwa wameweza kuelewa zaidi jinsi Akili Unde inavyoweza kubadilisha mazingira ya kazi, masomo na maisha kwa ujumla, huku wakihimizwa kujiandaa kuwa wabunifu na wachangiaji katika matumizi sahihi ya teknolojia hiyo. Kupitia mjadala huo, washiriki wameweza kupata uelewa wa kina kuhusu mwelekeo wa dunia katika nyanja ya AI na nafasi yao kama wataalamu wa baadaye katika kuhakikisha matumizi salama, jumuishi na yanayozingatia maadili ya teknolojia hii bunifu.