News-Details

News >Details

MZUMBE YAENDESHA WARSHA YA UWASILISHAJI WA TAFITI NA UDHAMINI WA MASOMO YA SHAHADA YA UZAMIVU KUPITIA MRADI WA SAfA

MZUMBE YAENDESHA WARSHA YA UWASILISHAJI WA TAFITI NA UDHAMINI WA MASOMO YA SHAHADA YA UZAMIVU KUPITIA MRADI WA SAfA

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe – Taaluma, Utafiti na Ushauri Prof. Hawa Tundui, amefungua rasmi warsha ya Uwasilishaji wa Tafiti na Udhamini wa Masomo ya Shahada ya Uzamivu (PhD unaofadhiliwa na Mradi wa SAfA. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo iliyofanyika chuoni Mzumbe, Prof. Tundui alieleza kuwa warsha hiyo ni sehemu muhimu ya kuonesha mchango wa mradi wa SAfA katika kukuza elimu ya juu na utafiti nchini, hasa kwa vijana. Alisisitiza umuhimu wa tafiti zinazojikita katika maeneo ya kilimo, afya ya jamii, usafirishaji na ugavi, pamoja na masoko. "Warsha hii ni jukwaa muhimu la kutathmini hatua iliyofikiwa na pia kuweka mikakati thabiti ya kuendeleza tafiti zenye tija kwa jamii. Tunathamini ushirikiano uliopo kati ya Mzumbe na taasisi zinazotekeleza mradi huu." alisema Prof. Tundui. Awali kabla ya kuanza kwa warsha hiyo, washiriki walipata fursa ya kumtembelea Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha ofisini kwake ambapo Prof. Mwegoha alieleza kuwa “Chuo Kikuu Mzumbe kina wataalamu wa kutosha katika sekta ya afya ya jamii, utawala, na kinaendelea kuimarisha ushirikiano wake na taasisi mbalimbali zikiwemo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kühne Foundation.” Aliongeza kuwa ni muhimu kupanua wigo wa ushirikiano huo ili kugusa maeneo mengine muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya vijana na taifa kwa ujumla. Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Kühne katika Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. Omary Swalehe, alisema kuwa SAfA ni mradi wa miaka minne ulioanza rasmi mwezi Mei 2023, unaotekelezwa na mashirika matatu yasiyo ya kiserikali ambayo ni DSW Tanzania, HRNS Tanzania, na KF Tanzania, katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Arusha na Kilimanjaro. Lengo kuu la mradi huo ni kuwajengea uwezo vijana kupitia mafunzo na programu za kuimarisha ujuzi. Mkurugenzi wa Kanda wa Kühne Foundation, Prof. Lester Brian Shawa, alikipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa utekelezaji mzuri wa mradi huo na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika nyanja mbalimbali.

None
None
None
None
None
None
None