News-Details

News >Details

WAFANYABIASHARA WADOGO WA MZUMBE WANUFAIKA NA MAFUNZO YA KODI NA UHASIBU

WAFANYABIASHARA WADOGO WA MZUMBE WANUFAIKA NA MAFUNZO YA KODI NA UHASIBU

Wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara zao ndani ya Chuo Kikuu Mzumbe wamenufaika na mafunzo ya muda mfupi yaliyoandaliwa na Idara ya Uhasibu na Fedha kwa lengo la kuwaongezea uelewa juu ya masuala ya kodi, tozo pamoja na misingi ya uhasibu na fedha. Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 11 Aprili 2025 na kufunguliwa rasmi na Amidi wa Skuli ya Biashara wa Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Gabriel Komba. Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Dkt. Komba alisisitiza kuwa elimu ya kodi na uhasibu ni nyenzo muhimu kwa wafanyabiashara wadogo kwani inawawezesha kusimamia biashara zao kwa tija, kufuata taratibu za kisheria na hatimaye kukuza mitaji yao kwa njia endelevu. Aliongeza kuwa Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Skuli ya Biashara, kitaendelea kushirikiana na jamii inayokizunguka kwa kutoa mafunzo ya vitendo yatakayosaidia kuinua uchumi wa wananchi. Mafunzo hayo yalitolewa na wataalamu wa ndani ya chuo wakiwa na uzoefu katika nyanja za fedha na kodi. Dkt. Joseph Kiria, Mhadhiri na Mkuu wa Idara ya Uhasibu na Fedha aliwasilisha mada kuhusu umuhimu wa mafunzo ya uelewa wa kodi na tozo, pamoja na misingi ya uhasibu na fedha kwa wafanyabiashara wadogo. Katika mada hiyo, alisisitiza umuhimu wa kuwa na utaratibu mzuri wa usimamizi wa fedha ili kuongeza uwazi na ufanisi katika biashara. Aidha, Mtoa Mada ambaye pia ni Mkufunzi Msaidizi CPA Kiburi Mwita, alitoa mada kuhusu aina mbalimbali za kodi na tozo zinazowahusu wafanyabiashara wadogo, akieleza kuwa uelewa wa aina hizo ni muhimu kwao ili kuepuka migongano na mamlaka za serikali. Mafunzo hayo yalihitimishwa kwa mada kutoka kwa CPA Oscar Mchaki, Mhadhiri Msaidizi, ambaye alifanya tathmini ya utekelezaji wa kodi na tozo kwa wafanyabiashara, akitoa mapendekezo ya namna bora ya kuboresha mifumo ya ulipaji wa kodi kwa sekta isiyo rasmi. Washiriki wa mafunzo walionesha shukrani kwa fursa hiyo na walipata nafasi ya kuuliza maswali, kubadilishana uzoefu na kupata majibu ya changamoto wanazokutana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None