News-Details

News >Details

MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU MZUMBE ASHIRIKI MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU MVOMERO

MAKAMU MKUU WA CHUO KIKUU MZUMBE ASHIRIKI MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU MVOMERO

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha ameungana na wananchi wa Wilaya ya Mvomero katika mapokezi ya Mbio za Mwenge wa Uhuru yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Sangasanga, Kata ya Mzumbe. Tukio hilo muhimu limefanyika katika eneo la ofisi ya Mtendaji wa Kijiji cha Sangasanga na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wa serikali, taasisi za elimu, wananchi, pamoja na wanafunzi kutoka maeneo ya jirani. Prof. Mwegoha aliambatana na baadhi ya watumishi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe, akiwemo Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo hicho Bw. Ally Maumbo, kama ishara ya kuunga mkono juhudi za kitaifa za kudumisha amani, mshikamano na uzalendo – maudhui yanayoasisiwa na Mbio za Mwenge wa Uhuru. Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka huu zinaendelea kubeba ujumbe wa kuwaelimisha na kuwakumbusha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi Mkuu kwa amani na utulivu ambao unatarajia kufanyika Oktoba Mwaka huu. Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe walieleza furaha yao katika kushiriki katika tukio hilo wakisema limetoa fursa ya kipekee kwao kushiriki katika shughuli za kijamii na kujifunza kuhusu uzalendo na mshikamano wa kitaifa. Chuo Kikuu Mzumbe kimekuwa mshiriki hai wa shughuli mbalimbali za kijamii katika Mkoa wa Morogoro, na ushiriki huu unaendelea kuonesha dhamira ya chuo katika kujenga uhusiano thabiti na jamii inayokizunguka.

None
None
None