News-Details

News >Details

MZUMBE YANG’ARA VIENNA KATIKA MASHINDANO YA KIMATAIFA YA USULUHISHI WA MIGOGORO YA KIBIASHARA

MZUMBE YANG’ARA VIENNA KATIKA MASHINDANO YA KIMATAIFA YA USULUHISHI WA MIGOGORO YA KIBIASHARA

Chuo Kikuu Mzumbe kimeweka historia kwa kushiriki na kung’ara katika mashindano mashuhuri zaidi duniani ya usuluhishi wa migogoro ya kibiashara – "The 32nd Willem C. Vis International Commercial Arbitration Moot" yanayofanyika jijini Vienna, Austria, barani Ulaya. Mashindano hayo yanahusisha vyuo zaidi ya 400 kutoka kote duniani, yamewakutanisha wanafunzi wa sheria kutoka maeneo mbalimbali duniani kujifunza na kuonesha umahiri wao katika sheria za usuluhishi wa kibiashara za kimataifa. Mzumbe imewakilishwa na timu mahiri ya wanafunzi wa Shahada ya Sheria ambao ni Bw. Abubakar Gembe, Bi. Neema Amon, Bi. Aichi Mvungi, Bi. Germana Sweke, Bi. Loraine Oloo na Bi. Latifa Njaa. Kwa mujibu wa Mratibu wa mazoezi ya kimahakama wa Chuo Kikuu Mzumbe kutoka Kitivo cha Sheria, Wakili Bernadetha Iteba, timu hiyo ilifanya maandalizi ya kina kwa muda mrefu ikiwa ni pamoja na kuandaa nyaraka za mawasilisho kwa pande zote mbili yaani mlalamikaji (Claimant) na mlalamikiwa (Respondent). Juhudi hizo zimezaa matunda baada ya timu ya Mzumbe kuibuka mshindi wa tuzo ya "Best Memorandum for the Claimant" kwa bara la Afrika – hatua iliyoiwezesha timu hiyo kufuzu hadi hatua ya robo fainali. Katika hatua ya robo fainali, timu ya Mzumbe ilishindana na vyuo vikongwe duniani likiwemo Chuo Kikuu cha Lapland kutoka Finland, Chuo Kikuu cha Zimbabwe, Chuo Kikuu cha Hannover kutoka Ujerumani, na Chuo Kikuu cha Miami kutoka Marekani. “Mafanikio haya ni kielelezo tosha cha ubora wa elimu ya sheria inayotolewa na Mzumbe pamoja na juhudi za walimu na wanafunzi wetu,” amesema Wakili Iteba. Mashindano haya yanaendelea na yanatarajiwa kufikia tamati tarehe 18 Aprili 2025. Ushiriki wa Mzumbe katika mashindano haya si tu unaleta heshima kwa chuo, bali pia unaiweka Tanzania katika ramani ya kimataifa ya elimu ya sheria na usuluhishi wa kibiashara.

None
None
None
None
None