News-Details

News >Details

WANAFUNZI MZUMBE DAR ES SALAAM WAPEWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ZA KISASA

WANAFUNZI MZUMBE DAR ES SALAAM WAPEWA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI NA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA ZA KISASA

Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kimeendesha mafunzo maalum kwa wanafunzi wake kwa lengo la kuwaongezea ujuzi katika maeneo muhimu ikiwemo ujasiriamali wa kisasa, matumizi ya teknolojia mpya, na mbinu za kuwavutia waajiri wa ndani na nje ya nchi. Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika Kituo cha Ndaki Upanga Dar es Salaam Tarehe 22 Aprili 2025 Mkuu wa Kitengo cha Kozi Fupi, Ubunifu na Ushauri wa Kitaalamu wa chuo hicho, Dkt. Darlene Mutalemwa, alieleza kuwa mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi kuelewa mahitaji halisi ya soko la ajira na namna ya kuyakidhi kwa ufanisi. “Kupitia mafunzo haya, wanafunzi walipata nafasi ya kujifunza ,kubadilishana uzoefu, na kukuza maarifa yao, jambo linaloongeza tija katika kazi na maisha yao ya kila siku,” alisema Dkt. Mutalemwa. Awali, Mwezeshaji wa Mafunzo kutoka Kampuni ya Peak Performance International, Tanzania ndugu Ikunda Kisimo alisema mafunzo hayo yatawaandaa washiriki kwa ajili ya ushindani wa soko la ajira la kimataifa kwa kuwajengea uwezo wa kiubunifu na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi. “Waajiri wa sasa wanahitaji wafanyakazi wanaozidi mipaka ya majukumu ya kawaida kwa watu wabunifu, wenye weledi wa kutumia teknolojia kuongeza tija kazini,” alisema Kisamo. Wanafunzi walioshiriki mafunzo hayo, walipongeza Uongozi wa Ndaki kwa kuwaleta wabobezi katika maswala mbalimbali na kueleza kuwa mafunzo hayo yamewapa uelewa mpana kuhusu umuhimu wa teknolojia na ubunifu katika mafanikio ya kikazi. “Katika dunia ya sasa, teknolojia ina nafasi kubwa katika mafanikio ya kazi yoyote. Mafunzo haya yamenifungua macho juu ya namna ya kutumia teknolojia kuongeza ufanisi wangu,” alisema Rebeca John, mwanafunzi wa Chuo hicho. Uongozi wa Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam umeahidi kuendelea kutoa mafunzo kama hayo mara kwa mara ili kuandaa jamii yenye maarifa, ubunifu, na uwezo wa kuchangia maendeleo chanya katika sekta mbalimbali nchini.

None
None
None
None
None