Chuo Kikuu Mzumbe kinaendelea na maandalizi ya Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali itakayofanyika kuanzia tarehe 07 hadi 09 Mei 2025, Kampasi Kuu Morogoro. Akizungumza na waandishi wa habari katika mkutano uliofanyika tarehe 25 Aprili 2025 – katika Ukumbi wa Multimedia wa Kituo cha Ubora katika Ufundishaji na Ujifunzaji wa Ubunifu, Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe – Morogoro, Meneja wa Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Uhusiano wa Kitasnia, Prof. Emmanuel Chao amesema tukio hilo litakuwa jukwaa muhimu kwa wanafunzi, jamii na wadau mbalimbali kujifunza, kushirikiana na kuonyesha ubunifu unaochochea maendeleo endelevu. “Tunalenga sio tu kusherehekea mafanikio ya Chuo Kikuu Mzumbe, bali pia kutoa fursa kwa vijana na jamii kushiriki katika mabadiliko ya kiuchumi kupitia ujasiriamali wa kisasa unaotegemea ubunifu,” amesema Prof. Chao. Lengo la mkutano huo na waandishi wa habari lilikuwa ni kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu tukio hilo, ambalo linatarajiwa kuvutia washiriki kutoka ndani na nje ya chuo, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa vyuo vingine, shule za sekondari, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wa maendeleo. Kwa mujibu wa Prof. Chao, Kambi ya Ujasiriamali itahusisha mafunzo kwa vitendo, maonesho ya bidhaa na huduma za ubunifu, midahalo, na mijadala ya kitaalamu itakayoongozwa na wataalamu wa sekta mbalimbali. Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali imekuwa tukio la kila mwaka lenye lengo la kukuza ubunifu, kukuza vipaji, na kuwaunganisha wanafunzi na fursa halisi za maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kwa mwaka huu tukio hili lina kaulimbiu isemayo: "Kupaa Zaidi ya Mipaka: Kuanda Kesho, Leo." @mzumbe_media @muso_updates @mzumbeuniversitydcc #mzumbeuniversity #mzumbeuniversitymbeyacampuscollege #mzumbedarcampus #mzumbeuniversitymorogoro #tujifunzekwamaendeleoyawatu