News-Details

News >Details

MZUMBE, TAKUKURU WAENDESHA SEMINA MAALUM YA KUPAMBANA NA RUSHWA KWA WANAFUNZI

MZUMBE, TAKUKURU WAENDESHA SEMINA MAALUM YA KUPAMBANA NA RUSHWA KWA WANAFUNZI

Chuo Kikuu Mzumbe Ndaki ya Dar es Salaam kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kimeendesha semina maalumu kwa wanafunzi wake, hususan wa Shahada ya Kwanza, iliyolenga kujenga uelewa kuhusu masuala ya rushwa, viashiria vyake, athari na mbinu za kuikabiliana. Akifungua semina hiyo katika kituo cha Ndaki hiyo Tegeta, Dar es Salaam tarehe 25 Aprili 2025, Mratibu wa Kituo hicho Dkt. Janeth Swai, aliwaasa wanafunzi hao kufuatilia kwa makini mafunzo hayo yaliyobeba dhana nzima ya maadili yenye kuelekeza kuishi kwa uadilifu ili kupelekea kuijenga jamii yenye tija na taifa Kwa ujumla. Naye Afisa Mchunguzi Mwandamizi kutoka TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Bi. Janeth Kafuko, aliwahimiza wanafunzi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa tangu wakiwa vyuoni ili kujenga jamii yenye misingi ya haki na uadilifu. Alisema kwa kulitambua hilo, TAKUKURU imekuwa na utaratibu endelevu wa kuanzisha Klabu za Kupambana na Rushwa Katika Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati na Shule (Anti-Corruption Clubs), ili kutanua uelewa wa wanafunzi tangu wakiwa katika masomo yao. “Tumeweka utaratibu endelevu wa kuanzisha Klabu za Kupambana na Rushwa katika vyuo vikuu, vyuo vya kati na shule mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu ya mapema kuhusu rushwa na athari zake katika jamii,” alifafanua Bi. Kafuko. Naibu Mshauri wa Wanafunzi wa Ndaki ya Dar es Salaam, Bi. Zitta Victoria Mnyanyi, alisema kuwa semina hiyo ni sehemu ya mkakati wa chuo kuhakikisha kila Mwanafubzi anaesoma Chuo Kikuu Mzumbe anapata maarifa ya kupambana na rushwa na kulea kizazi cha viongozi na wataalamu watakaotetea haki, uadilifu na kupinga rushwa kwa vitendo. “Rushwa ni janga linalohitaji kushughulikiwa kwa pamoja, mafunzo haya yana lengo la kuwapa wanafunzi zana za kutambua viashiria vya rushwa na namna ya kuepuka kujihusisha nayo katika maisha yao ya taaluma,” alisema Bi. Mnyanyi.

None
None
None
None
None
None