Chuo Kikuu Mzumbe kupitia kurugenzi yake ya afya kimezindua huduma ya kipimo cha ‘Ultra Sound’ ambayo imeanza kutolewa katika kituo cha afya cha chuo hicho kinachohudumia Wanafunzi, wafanyakazi na Wananchi wa kata ya Mzumbe na maeneo Jirani. Akizindua huduma hiyo Machi 19,2025 Kaimu Makamu Mkuu wa chuo kikuu Mzumbe ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa chuo anayeshughulikia Mipango, fedha na Utawala Prof.Allen Mushi amesema ununuzi wa mashine hiyo iliyogharimu kiasi cha shilingi 78,862,000/- kwa fedha za ndani ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya kwa kituo hicho ili kuhakikisha Wanafunzi, wafanyakazi na wanajamii wanaozunguka chuo wanapata huduma bora za afya kwa kwa uhakika “ Niwasihi Wanafunzi na Wananchi jirani wa maeneo yanayokizunguka chuo kuitumia huduma hii ambayo walikuwa wakiifuata mbali na sasa inapatikana hapahapa na pia inalipiwa kwa bima ya afya ama fedha taslimu“.Alisema Prof.Mushi Mkurugenzi wa huduma za afya chuo kikuu Mzumbe Dkt. Rajabu Nyagara amesema kuwa mashine hiyo ina uwezo mkubwa na inafanya kazi nyingi zikiwemo uchunguzi wa viungo vya ndani ya tumbo kama ini,mfuko wa nyongo na figo,uchunguzi wa viungo vya uzazi kwa wanawake ikiwemo mfumo wa njia ya mkojo,mji wa uzazi,mayai (ovary) na tezi dume kwa Wanaume Kazi nyingine ni kufuatilia maendeleo ya mtoto kwa Wajawazito,uchunguzi wa afya ya mishipa ya damu,uchunguzi wa umeme wa moyo na utendaji kazi wa moyo pamoja na afya ya misuli na viungo vingine. Dkt Nyagara amewakaribisha Wananchi wote kufika kwenye kituo cha afya Mzumbe kwa ajili ya kupata huduma zote hizo kutoka kwa Wataalamu mahiri waliopo kituoni hapo. Kwa upande wao wananchi wanaopata huduma katika kituo hicho wameishukuru Serikali na uongozi wa chuo kikuu Mzumbe kwa maboresho makubwa ya huduma za afya zinazoendelea kutolewa kituoni hapo na kusema kuwa huduma hiyo inasaidia kuwaondolea usumbufu kwani hapo awali iliwabidi kuifuata mjini ikiwa wameandikiwa kufanyiwa uchunguzi “Huduma hii kupatikana hapa kituo cha fya cha Mzumbe imetusarihisishia sana kwenye mlolongo wa matibabu,hasa sisi Wajawazito, kwani tulikuwa tukihudumiwa na madaktari wa hapa lakini ikifika hatua ya kupiga ‘ultra sound’ ilitubidi kuifuata mjini kilomita 30 kutoka hapa,tumefurahi sana kuletewa huduma hii karibu”.Alisema Aisha Hussein, mkaazi wa Kijiji cha Changarawe kilichopo kata ya Mzumbe.