Warsha maalumu ya watoa huduma (wadau) wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) imefanyika Kampasi Kuu, Chuo Kikuu Mzumbe, tarehe 21 Machi 2025, ikiwakutanisha waratibu wa mradi wa HEET Chuo Kikuu Mzumbe na watoa huduma mbalimbali kwa lengo la kuwaelimisha katika maeneo ya Miundombinu, Mazingira, Jinsia, Jamii, Afya na Usalama pia kuwashirikisha katika utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unafanikishwa kwa ufanisi. Akifungua Warsha hiyo, Kaimu Naibu Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) katika Chuo Kikuu Mzumbe Dkt. Lihoya Chamwali, alisema lengo la warsha hiyo ni kuwaelimisha wadau walioshiriki ambao ni viongozi wa serikali, maafisa utumishi, wataalamu wa mazingira, wawakilishi wa jamii, wahandisi wa miundombinu pamoja na wataalamu wa jinsia na afya katika utekelezaji wa mradi huo. Naye Mratibu wa mradi wa HEET Kwa upande wa miundombinu, ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Miliki wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Joseph Ng'wala, alieleza hatua zilizofikiwa katika ujenzi wa majengo mapya. Naye Mratibu wa HEET upande wa mazingira, Dkt. Editha Ndunguru, aliwasilisha mada kuhusu nguzo kuu za Benki ya Dunia, akisisitiza uzingatiaji wa viwango vya kimazingira katika utekelezaji wa mradi huo. Kwa upande mwingine, Mratibu wa HEET upande wa jinsia na mahitaji maalumu, Dkt. Perpetua Kalimasi, alizungumzia unyanyasaji wa kijinsia na kingono kwa watoa huduma, akihimiza kuwepo kwa mifumo ya kuzuia ukatili wa kijinsia. Naye Mratibu wa HEET anayehusika na kudhibiti athari za mradi kwa jamii, Dkt. Christina Shitima, alieleza taratibu za usimamizi wa malalamiko, akisisitiza uwazi na ushirikishwaji wa jamii. Kwa ujumla, warsha hii imeonesha dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kuhakikisha wadau wake wanapata uelewa wa kina kuhusu mradi wa HEET. Kwa upande mwingine, viongozi wa serikali na maafisa utumishi walioshiriki walielezea kuridhishwa kwao na hatua zinazochukuliwa katika utekelezaji wa mradi huo. Mwisho, Dkt. Chamwali aliwashukuru washiriki kwa mchango wao na kuwataka kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha mradi wa HEET unatekelezwa kwa mafanikio.