Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe (Mb.), amekipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuwatengenezea mazingira wanafunzi wa chuo hicho yanayohamasisha ubunifu, kujifunza mbinu za Ujasiriamali, uwekezaji na Biashara wakati wakiendelea na masomo yao chuoni hapo na hivyo kuwaandaa vyema kujiajiri na kutatua changamoto ya ajira na kuwawezesha kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa Mhe. Kigahe ameyasema hayo wakati akimuwakilisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo (Mb.), katika maadhimisho ya siku ya Chuo Kikuu Mzumbe na kambi ya Ujasiriamali iliyofanyika Mei 8,2025 Kampasi Kuu Morogoro na kuwataka wanafunzi hao kuitumia fursa hiyo vizuri kwa kufanya bunifu zinazoendana na kukua kwa teknolojia zitakazowezesha kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii na kuiwezesha Tanzania ya viwanda inayojitegemea kwa maarifa na teknolojia. "Nimefurahishwa sana na tukio hili kwani inaonesha namna Chuo kikuu Mzumbe kinavyotekeleza kwa vitendo agenda ya Serikali ya kutaka vijana kupatiwa elimu na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri, kwani tumeona hivi karibuni Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amezindua sera mpya ya elimu inayotaka Vijana kupatiwa mafunzo ya amali, lakini pia hivi karibuni Mhe. Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa Watanzania kwenda kusoma VETA".Alisema Aidha, Naibu Waziri aliongeza kuwa chuo Chuo Kikuu Mzumbe kimekuwa kikitambulika kwa umahiri katika kufundisha masomo ya utawala na Menejimenti lakini sasa kimechukua hatua madhubuti kwa kuibeba agenda ya kujenga ujuzi na kuwapa vijana fursa za ubunifu kwa vitendo na kuwaomba kuendeleza programu hiyo kwakuwa ni jukwaa muhimu sana katika kuvumbua vipaji vya ubunifu kwa manufaa ya taifa zima Kwa upande wake Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango anayeshughulikia masuala ya ubunifu wa biashara, Dkt. Lorah Basolile Madete, alikipongeza Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuandaa tukio na kuongeza kuwa kaulimbiu ya mwaka huu inaonyesha namna ambavyo vijana wanatakiwa kuziendea ndoto zao bila kuangalia vikwazo na mipaka na kwamba kambi kama hizo ni jukwaa la kulea na kukuza Wajasiriamali wengi wa sasa na wa baadaye kutoka ndani ya jamii. Awali Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Hawa Tundui ambaye pia ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri alisema kuwa kambi hiyo imekuwa sehemu ya utamaduni wa kila mwaka wa Chuo Kikuu Mzumbe ambapo lengo lake ni kuwajengea wanafunzi uwezo wa ubunifu na kuwahamasisha kuanzisha miradi ya kiuchumi itakayosaidia kuleta maendeleo katika jamii. Katika tukio hilo, Naibu Waziri alipata fursa ya kutembelea mabanda ya wanataaluma, wajasiriamali, na wabunifu, pamoja na kushuhudia mashindano ya uwasilishaji wa wazo la kibiashara ambapo washiriki walieleza mawazo yao ya kibunifu na kushindanishwa ambapo bi.Edna Laizer mwanafunzi kutoka kitivo cha Sayansi na Teknolojia (FST) aliibuka mshindi wa kwanza kwa kubuni kifaa cha kuchuja maji kwa matumizi ya vijiji na mijini Katika hatua nyingine Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, alisisitiza dhamira ya Chuo Kikuu Mzumbe kuendelea kuwa jukwaa la kukuza vipaji, ubunifu na ujasiriamali wa vijana kwa maendeleo endelevu ya Taifa na kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhakikisha Vijana wanapatiwa elimu na ujuzi utakaowawezesha kujiajiri.