Chuo Kikuu Mzumbe kimeanza rasmi Kambi ya Ujasiriamali kwa shamrashamra za bonanza la michezo lililofanyika tarehe 7 Mei 2025, likihusisha michezo ya aina mbalimbali ambayo ilileta burudani na mshikamano miongoni mwa wanafunzi na watumishi wa chuo. Bonanza hilo lilifunguliwa rasmi na Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof. Hawa Tundui, ambaye alisisitiza umuhimu wa kushiriki michezo kwa ajili ya kuimarisha afya, kuhimiza ushirikiano na kujenga ari ya ushindani. “Michezo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha afya ya mwili na akili, lakini pia hujenga mshikamano unaohitajika katika mazingira ya kujifunza na kufundisha,” alisema Prof. Tundui. Katika michezo hiyo ya kuvutia, timu ya mpira wa miguu ya wanafunzi iliibuka kidedea dhidi ya timu ya watumishi kwa ushindi wa bao 1-0 goli pekee likifungwa na Tibaigana Alfred, Mwanafunzi kutoka Skuli ya Utawala na Menejimenti (SoPAM). Katika mpira wa wavu upande wa wanawake, watumishi waliibuka na ushindi wa seti 3-0 dhidi ya wanafunzi. Michezo mingine iliyofanyika ni pamoja na mbio fupi za mita 100, kukimbia na gunia, kukimbiza kuku, kukimbia na yai pamoja na mashindano ya kukuna nazi, ambapo watumishi walionyesha umahiri na kuibuka na ushindi. Bonanza hilo pia lilishuhudia uzinduzi rasmi wa "Mzumbe Jogging Club" kikundi kipya cha mazoezi ya kukimbia kilichoanzishwa kwa lengo la kuimarisha afya, kuleta umoja na kuongeza ari ya mazoezi miongoni mwa wanajumuiya wa chuo. Washindi wa michezo mbalimbali walitunukiwa medali na makombe na mgeni rasmi Prof. Hawa Tundui. Bonanza lilihitimishwa rasmi na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Mipango, Fedha na Utawala, Prof. Allen Mushi, ambaye alipongeza washiriki wote kwa ushiriki wao na kuhimiza kuendelezwa kwa utamaduni wa michezo chuoni. “Michezo si tu burudani bali ni sehemu ya kuimarisha utendaji, afya na mshikamano wa pamoja katika taasisi ya elimu ya juu,” alisema Prof. Allen Mushi. Kambi ya Ujasiriamali inaendelea hadi Mei 9, 2025, ikitarajiwa kuwa jukwaa la mafunzo, ubunifu na maendeleo ya ujuzi wa wanafunzi wa Mzumbe.