Wanafunzi na wahitimu wa vyuo mbalimbali walikusanyika tarehe 11 Mei 2025, Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro kwenye tukio la Majadiliano Kuhusu Fursa na Mbinu za Ajira (Career Fair), lililofanyika kwa ushirikiano kati ya Niajiri Platform na Association Internationale des Étudiants en Sciences Économiques et Commerciales (AIESEC). Tukio hili lililenga kuwawezesha vijana kujifunza mbinu za kufanya usaili wa haraka (speed interviews) kwa ajili ya fursa za mafunzo ya vitendo na ajira, kuunganishwa na waajiri na wataalamu wa sekta mbalimbali, na kuimarisha ujuzi wa ajira, ujuzi wa kidijitali na kifedha. Tukio hili liliwavutia wazungumzaji mbalimbali waliotoa mada juu ya uongozi, ujuzi wa kuajirika, na umuhimu wa vijana kujitokeza kwenye fursa za kitaaluma na ajira. Wazungumzaji walijikita katika kuchochea ari ya uongozi miongoni mwa vijana na kuwahamasisha kutumia fursa zinazotolewa na majukwaa kama Niajiri na AIESEC kwa maendeleo ya kitaaluma na kijamii. Awali, Rais wa AIESEC Mzumbe Bw. Hassan Mapezi alisisitiza umuhimu wa vijana kuchukua jukumu la kuleta mabadiliko, nguvu ya uongozi, na umuhimu wa kujitokeza kwenye fursa zinazoweza kubadilisha maisha yao ya baadaye. Alieleza kuwa uongozi wa vijana unaleta mabadiliko chanya na kushiriki kwenye matukio kama haya ni hatua muhimu kuelekea mafanikio. Naye, Bw. Mrisho Kagoha kutoka Niajiri Platform aliwaeleza washiriki juu ya umuhimu wa Uniconnect na Career Fair kama majukwaa muhimu ya kuwaunganisha vijana na waajiri, huku akitoa mwongozo wa mbinu bora za kujitokeza katika soko la ajira. Alihimiza washiriki kutumia fursa kama hizi kwa manufaa ya maendeleo ya kitaaluma na kiujuzi. Aidha, Mkurugenzi wa AIESEC Tanzania, Bw. Vicent Manila alibainisha kuwa uongozi wa vijana ni chachu ya maendeleo na kuwa majukwaa kama haya yanawasaidia vijana kuwa viongozi wenye kuleta mabadiliko. “Vijana ni nguvu ya sasa na mustakabali wa kesho. Kujitokeza kwenye matukio kama haya ni uwekezaji wa kujenga mustakabali bora,” alisema Bw. Manila. Washiriki wa Majadiliano Kuhusu Fursa na Mbinu za Ajira (Career Fair) walionyesha kuridhishwa na maudhui ya tukio hilo, wakibainisha kuwa limewapa mwangaza mpya kuhusu ujuzi wa kuajirika na jinsi ya kujiandaa kwa mahojiano ya kazi. Tukio hili limeacha alama muhimu kwa vijana waliohudhuria kwa kuwapa fursa ya kujifunza na kujipanga kwa safari ya ajira na uongozi.