News-Details

News >Details

SIKU YA MZUMBE NA KAMBI YA UJASIRIAMALI 2025 YAFANA

SIKU YA MZUMBE NA KAMBI YA UJASIRIAMALI 2025 YAFANA

Chuo Kikuu Mzumbe kupitia Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Uhusiano wa Kitasnia, kimeadhimisha Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali katika Kampasi Kuu ya Morogoro, tarehe 7 Mei 2025 na kuhudhuriwa na washiriki kutoka sekta mbalimbali za elimu, biashara, uwekezaji na taasisi za serikali. Akizungumza wakati wa tukio hilo, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Hawa Tundui, alisisitiza kuwa tukio hilo linaendana na mkakati wa chuo wa kukuza elimu ya vitendo, ubunifu na ujasiriamali kama nyenzo ya kujenga uchumi shindani unaotegemea maarifa. Alieleza kuwa kupitia kambi hiyo, washiriki watapata nafasi ya kuibua mbinu mpya za kujiajiri na kuanzisha biashara zenye tija. Kwa upande wake, Meneja wa Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Uhusiano wa Kitasnia – Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Emmanuel Chao, alieleza kuwa Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali ni sehemu ya juhudi endelevu za chuo kuwa kiungo kati ya taaluma na jamii, kwa kukuza ushirikiano wa kimkakati kati ya wanafunzi, sekta binafsi na wadau wa maendeleo. Aidha, tukio hilo lilipewa heshima ya kipekee na Mwakilishi wa Shirika la Global Expert Bureau, Bw. Kabeho Solo, ambaye alikabidhi nakala 50 za kitabu cha “The Business of People” kwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Taaluma, Utafiti na Ushauri wa Kitaaluma – Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Hawa Tundui, kama mchango wa maarifa kwa maendeleo ya elimu na uongozi wa kijamii. Vilevile, washiriki walifaidika na mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalamu waliobobea katika maeneo ya ujasiriamali na uwekezaji. Miongoni mwao alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la TAOTIC, Bw. Kiko Kiwanga, aliyezungumzia mada kuhusu “Uchaguzi wa Taaluma na Mustakabali wa Ajira: Ujasiriamali wa Kijamii Unaotegemea Ubunifu”, ambapo alisisitiza umuhimu wa vijana kujitambua na kutumia changamoto kama fursa za kujiajiri. Kwa upande mwingine, Afisa wa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Bw. Oswald Y. Karadisi, aliwasilisha mada kuhusu fursa mbalimbali zinazotolewa na baraza hilo katika kuwawezesha wananchi kiuchumi. Alihimiza washiriki kujitokeza kwa wingi katika programu za mafunzo, mitaji na uungwaji mkono wa kitaalamu. Sambamba na hayo, Afisa Uwekezaji kutoka Taasisi ya Uwekezaji ya (UTT AMIS), Bw. Fredric P. Lushinge, aliwasilisha mada kuhusu fursa za uwekezaji zinazotolewa na mfuko huo, akieleza umuhimu wa vijana kuanza kupanga maisha yao kifedha kwa kuwekeza mapema katika bidhaa salama na zenye manufaa ya muda mrefu. Siku ya Mzumbe na Kambi ya Ujasiriamali imeonesha dhamira ya dhati ya Chuo Kikuu Mzumbe katika kuwa kiungo muhimu kati ya taaluma, ubunifu na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia ushirikiano kati ya vijana, taasisi za kifedha, mashirika ya maendeleo na sekta binafsi. Chuo Kikuu Mzumbe, Tujifunze Kwa Maendeleo ya Watu.

None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None
None