Mafunzo kuhusu fursa mbalimbali za kijasiriamali yametolewa mwishoni mwa wiki na wadau mbalimbali wa ujasiriamali katika muendelezo wa kusherehekea siku ya Chuo kikuu Mzumbe na kambi ya ujasiriamali. Mkurugenzi wa TAOTIC bw Kiko Kiwanga akielezea kazi mbalimbali zinazofanywa na taasisi yake kama njia ya kumsaidia kijana mjasiriamali, alisema; wao wamejikita zaidi katika kuibua, kulea na kusaidia utendaji wa biashara jamii (biashara zilizojikita kutatua changamoto mbalimbali za kijamii). Pia aliwasihi wanafunzi hao kujiunga na mtandao wa ujasiriamali wa vyuo vikuu ambao wao ndio waanzilishi kwani humo kuna fursa nyingi sana kwa wanafunzi walioko vyuoni na wale waliohitimu. Kwa upande wake bw Ismail Juma muwakilishi toka SAHARA VENTURE, naye alielezea kazi mbalimbali zinazofanywa na taasisi yake ambazo ni kulea wazo la biashara, kutoa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali na kuunganisha wajasiriamali na watu wenye mitaji. Alisisitiza kuwa jambo la muhimu sana kufanikiwa kwenye ujasiriamali ni kuwa na wazo zuri la biashara na sio mtaji kwani wako wengi wenye mitaji wanatafuta watu wenye mawazo mazuri ili waweze kuwekeza pesa zao. Pia alizungumzia mambo matano muhimu ili mtu afanikiwe kibiashara ambayo ni kuwa na akili ya ubunifu, ujuzi wa vitendo, ushauri na mshauri mzuri, wateja na nidhamu binafsi. Aidha muwakilishi toka Golden star Consultants Bw Zephania Philemon naye alielezea fursa mbalimbali za nje ya nchi walizonazo ambazo ni mafunzo tarajali (kwa wanafunzi walioko masomoni na waliohitimu) na ufadhili wa masomo kuanzia ngazi ya cheti mpaka shahada ya uzamivu. Pia alielezea vitu vinavyohitaji ili kupata fursa ya ufadhili na mafunzo tarajali. Kwa kumalizia alielezea umuhimu wa wanafunzi wetu kutumia hizi fursa za nje ikiwa ni pamoja na kupata uzoefu wa namna wenzetu wanavyofanya kazi zao ili watuletee uzoefu huu nchini kwa maendeleo ya taifa letu. Kwa upande mwingine, mwakilishi kutoka SUGECO Bi. Jackline Jonathan naye alieleza fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye taasisi hiyo ambazo ni kulea na kuatamia biashara, kuleta mabadiliko ya mawazo (kilimo kinaanzia sokoni na sio shambani), fursa za mafunzo tarajali, ushauri na mafunzo, ufungaji wa nyumba za kijani, sakafu kavu na kutoa mahali pa kufanyia uzalishaji. ‘’Ingawa SUGECO ilianzishwa maalumu kwa ajili ya wanafunzi na wahitimu wa SUA, sasahivi imepanua wigo wake na kumfikia kila kijana wa kitanzania, hivyo karibuni wote SUGECO’’ alisisitiza bi Jackline. Alihitimisha kwa kuelezea ili uwe mjasiriamali mwenye ushindani lazima upende kupata ujuzi mbalimbali ikiwemo uongozi na masiliano, pia ni lazima uweze kubadilika kulingana na mabadiliko ya mazingira ya kibiashara hususan kwenye teknolojia Pia wanafunzi walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali kwa wawezeshaji wote na kupatiwa majibu ya kuridhisha kabisa. Chuo kikuu Mzumbe, tujifunze kwa maendeleo ya watu