Katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe wanahitimu elimu ya juu wakiwa na uwezo wa kujiajiri, kuanzisha biashara endelevu ili kuchangia kikamilifu maendeleo ya uchumi wa taifa, Chuo Kikuu mzumbe kupitia mradi wa HEET kimeandaa warsha maalum ya kuamsha na Kulinda bunifu na Ujuzi wa Biashara kwa wanafunzi wa Ndaki ya Mbeya. Warsha hii inafanyika kuanzia tarehe 13-16 Mei, 2025 jijini Mbeya. Warsha hii inalenga kuhamasisha wanafunzi katika umuhimu wa ubunifu, ulinzi wa miliki bunifu (Intellectual Property/IP), na ujuzi wa msingi wa biashara (business essentials). Lengo kuu likiwa ni kutoa maarifa kwa wanafunzi, kutoa maarifa na mbinu za kisasa katika kuwezesha kubuni, kulinda na kuendeleza mawazo ya kibunifu hadi kufika hatua ya kuwa biashara rasmi. Akifungua warsha hiyo, Prof. Henry Mollel, Rasi wa Ndaki ya Mbeya aliwahimiza wanafunzi kuelewa kuwa dunia ya sasa inahitaji fikra mpya,suluhisho mbadala na ujasiri wa kuanzisha biashara hivyo, wahakikishe mpaka mwisho wa warsha hiyo wawe wameongeza kitu. “Ajira sio tegemeo pekee, bali uwezo wa kubuni na kuanzisha miradi ya kijamii na kibiashara ndio mwelekeo wa maendeleo. Mafunzo haya yawasaidie kufikiri kwa upana, kuchambua changamoto kama fursa na kuwa wabunifu;” alisema Prof. Mollel. Naye, Prof. Emmanuel Chao, Meneja wa Kitengo cha Ubunifu, Ujasiriamali na Uhusiano wa Kitasnia alieleza kuwa kwa muktadha wa soko la ajira linalobadilika kwa kasi, ni muhimu kwa wanafunzi kufahamu mbinu za ubunifu na biashara ili kuweza kujitegemea baada ya kuhitimu masomo yao. Aliongeza kuwa, kwa kutambua hayo Chuo kimeanzisha kitengo maalum cha kulea bunifu za wanafunzi ambacho kinawezesha wanafunzi kukuza mawazo yao na kupatiwa haki miliki ili kulinda bunifu kisheria. Kwa upande wake Dkt. Christina Shitima, Mratibu wa Mradi wa HEET upande wa Tafiti na Ubunifu alisema kuwa mradi huu unaunga jitihada za kukuza bunifu chuoni. Pia, alisisitiza kuwa warsha hii hailengi wanafunzi wenye mawazo ya bunifu pekee, bali pia ni fursa kwa wasio na mawazo ili waweze kuhamasika kuibua fikra mpya na kuweza kuwa wabunifu bora zaidi. Aidha, Dkt. Irene Shubi Isibika, Mratibu wa Kitengo cha Ubunifu na Uatamiaji aliwasisitiza wanafunzi kutumia nafasi hii kuleta mawazo yao ya biashara na teknolojia kwa ajili ya kupatiwa ushauri wa kitaalamu wa kuendeleza mawazo hayo. “Kitengo cha Ubunifu kipo kwa ajili yenu, ni chumba cha kutengeneza ndoto zenu. Lilete wazo lako kama ni biashara, huduma ya jamii au bidhaa mpya nasi tutakusaidia kulilea, kuliboresha na hatimaye kulifanya kuwa kubwa na kuleta tija katika jamiii zetu.” Alisema Dkt. Isibika. Kwa ujumla, warsha hii ni sehemu ya mkakati mpana wa Chuo Kikuu Mzumbe kuhakikisha kuwa mwanafunzi anakuwa na uelewa wa kina kuhusu mchakato wa kubuni, kulinda na kuendeleza biashara na miradi bunifu ili kuleta chachu katika maendeleo ya uchumi, uwekezaji na viwanda.