Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha, ametembelea na kukagua miradi ya maendeleo na uboreshaji wa miundombinu katika Kampasi Kuu ya Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro. Ziara hiyo ilifanyika tarehe 20 Mei 2025, ambapo aliambatana na viongozi mbalimbali wa Menejimenti ya Chuo. Katika ziara hiyo, Prof. Mwegoha alitembelea miradi mbalimbali ikiwemo uboreshaji wa viwanja vya michezo, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya mikahawa, barabara za ndani ya chuo, ujenzi wa jengo la huduma za upasuaji katika kituo cha afya cha chuo, pamoja na ujenzi wa majengo mapya ya Taaluma na TEHAMA katika eneo la Maekani. Akizungumza wakati wa ukaguzi huo, Prof. Mwegoha alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa, kwa kuzingatia vigezo vya kitaalamu kutoka kwa wahandisi na wataalamu wa miliki wa Chuo Kikuu Mzumbe. Aliahidi kuwa Menejimenti itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha wakandarasi wanapata mazingira bora ya kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. “Jambo la msingi ni kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaokusudiwa. Sisi kama Menejimenti tupo tayari kuendelea kutoa ushirikiano unaohitajika katika kila hatua ya utekelezaji wa miradi. Tutakuwa tukifanya ufuatiliaji wa mara kwa mara ili kuona maendeleo na kushughulikia changamoto zitakazojitokeza,” alisema Prof. Mwegoha. Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Miliki wa Chuo Kikuu Mzumbe, Bw. Wolta Shio, aliwapatia viongozi wa Menejimenti taarifa ya hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, pamoja na makadirio ya muda wa kukamilika kwa kila mradi. Prof. Mwegoha alihitimisha ziara yake kwa kuwataka watendaji wote wanaohusika na miradi kuhakikisha wanaendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kushirikiana ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa wakati.